Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Thabo Mbeki amewataka waafrika kuwaenzi mashujaa waliopambana kwa ajili ya uhuru wa nchi zao ili kutunza historia hiyo iliyotukuka kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Rais huyo mstaafu amesema hayo Mei 22, 2025, wakati wa ziara maalum kutembelea eneo la kihistoria la Mazimbu Mkoani Morogoro ambapo wamezikwa wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini Mkoani humo waliokuwa uhamishoni wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi wa taifa hilo
Rais Thabo Mbeki amesema, ni jukumu letu nchi za kiafrika kuwaenzi mashujaa waliopoteza maisha katika harakati za kusaidia ukombozi wa nchi zao ili kuweza kulinda historia za mashujaa hao kwa vizazi na vizazi.
Aidha, kiongozi huyo amesema ameguswa na juhudi za Tanzania kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kazi kubwa ya kulinda na kuyatunza maeneo hayo ya kihistoria ya wapambanaji kwani hali hiyo inaonyesha mshikamano na uhusiano mzuri wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru kiongozi huyo kwa kuja Morogoro na kutembelea makaburi ya mashujaa hao jambo ambalo linajenga utu kwa kuwakumbuka mashujaa waliopigania Uhuru wa Taifa lao.
Ziara ya Mhe. Thabo Mbeki Mkoani Morogoro ni sehemu ya Maadhimisho ya siku ya Afrika ambapo huazimishwa kila mwaka Mei 25, kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (zamani OAU) na kuhamasisha mshikamano, maendeleo na utambulisho wa bara la Afrika.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.