Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo ametoa Ombi kwa niaba ya TARURA Mkoa wa Morogoro kuongezewa fedha kwa ajili ya Taasisi hiyo Mkoani humo kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.
Mhandisi Kalobelo amewasilisha ombi hilo Disemba 3 mwaka huu mbele ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara hapa nchini (Road Board Fund) walipofika Ofisini kwake kujitambulisha kuwa wapo Mkoani humo kwa ziara ya siku moja ya kutembelea taasisi za TARURA na TANROAD.
Amesema, Mkoa wa Morogoro una changamoto nyingi za barabara hususan za vijijini kwa sababu ya ya mkoa kuwa na Milima na Mabonde kunapelekea uwepo wa madaraja na makaravati mengi, kati ya hayo mengi huharibika kipindi cha masika hivyo, amewaomba wajumbe kupokea maombi ya TARURA Mkoa wa Morogoro ya kuongezewa bajeti mara watakapowasilisha maombi yao kwao kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.
“Naomba niwasilishe rasmi pale ambapo wataomba kuongeza ongeza keki ya uhitaji wa fedha, naomba muwafikirie. Kwa sababu hawa sasa ndio wanaohudumia barabara sio za mijini peke yake lakini hata zinazokwenda kwenye uzalishaji” amesema Mhandisi Kalobelo.
Aidha, Katibu Tawala huyo wa Mkoa ameipongeza Serikali kwa kuanzisha chombo cha kushughulikia barabara, yaani TARURA. Amesema huo ni utaratibu mzuri na ana imani kuwa kwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo kutakuwa na mafanikio mazuri zaidi katika sekta ya miundombinu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Joseph Haule amewataka Mameneja wa TARURA hapa nchini kuwa na utamaduni wa kuweka kwenye bajeti kazi zote zinazotakiwa kufanyika ndani ya kipindi husika zikitanguliwa na kazi ambazo ni vipaumbele vyao, badala ya Mameneja hao kuomba fedha kwa mtindo wa dharura hali inayopelekea kuwa ni vigumu kutoa fedha hizo kwa vile haziko kwenye bajeti zao.
Maelezo hayo ya Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara yalikuja baada ya Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Benjamin Maziku na Mhandisi wa Barabara na Meneja wa TARURA wa Halamshauri ya Manispaa ya Morogoro Mhandisi Macknon Nkwera kuomba kuongezewa fedha za Dharura kutokana na miundombinu mingi kuharibika hususan wakati wa Masika.
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wapo Mkoani Morogoro kwa ziara ya siku moja kutembelea Taasisi za TARURA na TANROAD Mkoa wa Morogoro ili kuona kazi wanazozifanya, changamoto wanazokumbana nazo na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Taasisi hizo mkoani humo.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.