RC Malima awataka Maafisa Tarafa, watendaji wa Kata kuwajibika.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kuwajibika kufanya kazi kwa kujitambua katika maeneo yao ili waweze kuwaletea maendeleo wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa tarafa na watendaji wa kata wa Mkoa wa Morogoro kata yaliyofanyika katika ukumbi wa mbarak mwinshehe uliyopo halmashauri ya manispaa ya Morogoro.
".. ninachotaka kutoka kwenu ni ubunifu, kujituma, muonekane kuwa mnajua mnachofanya, usimamizi wa miradi.." Amesisistiza Mhe. Malima
Aidha, amesema kuna umuhimu mkubwa wa maafisa hao kujua majukumu yao vilivyo na kufanya kazi kwa kujituma, kujitoa na kufanya usimamizi mzuri katika miradi ya maendeleo kwa maslahi mapana ya Taifa na sio kwa maslai yao binafsi.
Pia kiongozi huyo amesema moja ya changamoto inayowakabili maafisa hao ni kutokuwa na ubunifu katika utendaji kazi wao hivyo amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa kata wawe wabunifu ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo wanayosimamia.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima amewataka watendaji hao wa Serikali kujituma na kusimamia miradi ya maendeleo kwa kuwa ni jukumu lao la kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakamilika kwa wakati lakini ikiwa na ubora unaohitajika.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Simoni maganga amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa na Watemdaji wa Kata ili kuweza kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yalianza Juni 6, 2023 katika Mikoa ya Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa na kubakiza Mikoa nane ambayo yatafanyika kwa mwaka wa fedha 2024/ 2025.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.