Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo kufuatilia fedha zilizotumwa na Serikali kwa ajili ya Ujenzi wa bwalo la shule ya Sekondari Gairo, ambalo hadi sasa halijakamilika huku Serikali ikiwa imetuma shilingi milioni mia moja.
Loata Sanare ametoa maagizo hayo Disemba Mosi mwaka huu wakati wa ziara yake Wilayani humo na kufanya kikao katika ukumbi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Gairo na kuhusisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Wakuu wa Idara, Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari na watendaji wengine wa Serikali.
Katika maelezo yake Mkuu huyo wa Mkoa amebanisha kuwa, zaidi ya shilingi milioni mia moja zimetumwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Bwalo la shule ya Sekondari ya Gairo, lakini hadi sasa jengo hilo haljakamilika na kiasi cha fedha kilichotumika ni zaidi ya shilingi milioni tisini.
Kwa sababu hiyo, Loata Sanae amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kuunda kamati itakayofuatili undani na ukweli wa matumizi ya fedha za mabweni ya shule Nne za Sekondari Wilayani humo likiwemo bweni la shule ya sekondari ya Gairo ili kujua kama kuna ukiukwaji wa matumizi ya fedha zilizotolea ili wahusika waliohujumu Mradi huo wachukuliwe hatua za kisheria.
“hawa wa Idara ya Elimu Mkoani wapo hapa, mtamwona RAS asubuhi atafute Kamati ya kufuatilia fedha zilizoletwa Gairo kwa ajili ya hosteli hizo, tujue zimeletwa shilingi ngapi na status (hali ya ujenzi) ya kazi ikoje. Kama zinaendelea vizuri tuhakikishe tunasukuma ili kazi imalizike mara moja” alisema Sanare.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza Viongozi wa Wilaya hiyo kupokea maagizo ya Serikali na kuyatekeleza ikiwa ni pamoja na agizo la Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kutaka kila Mkoa kuwa na shule moja ya Sekondari ya Sayansi kwa ajili ya watoto wa kike huku yeye akitoa maelekezo kwa kila Wilaya kuwa na sekondari hizo kwa kuwa uwezo upo.
Katika hatua nyingine, Loata Ole Sanare ameagiza kushughulikiwa kwa nguvu kesi za mimba mashuleni kwa watuhumiwa kufikishwa Mahakamani na kuchukuliwa hatua zinazostahili, ambapo hadi sasa Wilaya ya Gairo ni kinara wa mimba za utotoni katika Mkoa huo, kwa kuwa na jumla wanafunzi zaidi ya 100 waliokatishwa masomo kwa sababu ya mimba za utotoni kwa Shule za Msingi na Sekondari.
“Kesi za ubakaji na mimba mashuleni ni nyingi sana na mnasema zipo Polisi na Mahakamani lakini hakuna hata moja tulioshinda hadi sasa, na kesi zingine hazijapelekwa Mahakamani, eti bado uchunguzi unaendelea, pia sehemu nyingine hata watuhumiwa hawakukamatwa, mnafanya kazi gani sasa?” alihoji Loata Sanare.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Siriel Mchembe akitoa taarifa fupi kwa Mkuu wa Mkoa amesema changamoto ya mimba mashuleni ni kubwa katika Wilaya yake huku akitoa mfano wa tatizo hilo kwa kipindi cha miezi miwili ya CORONA walipata kesi zaidi ya 100 ya wanafunzi waliopata mimba.
Amebainisha kuwa sababu kubwa ya changamoto hiyo ni taarifa za wanafunzi wanaopata mimba kuchelewa kuwafikia viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya, umbali mrefu wa huduma ya mahakama na wazazi wa pande mbili kukubaliana kumaliza tatizo hilo kienyeji, hivyo ametoa wito kwa wananchi, na wazazi kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kukomesha tatizo hilo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.