Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg. Gerald Kusaya ametoa wito kwa wakulima wote nchini kukata Bima ya mazao ili iwakinge na maafa mbalimbali na kuwapa uhakika na usalama wa shughuli zao kabla na baada ya kupata maafa yatokanayo na changamoto za kilimo.
Ndg. Kusaya ametoa wito huo Disemba 11, mwaka huu wakati wa hafla ya malipo ya fidia kwa wakulima watano kupitia shirika la bima la Taifa (NIC) waliopata hasara ya mazao kutokana na majanga mbalimbali iliyofanyika katika Ofisi za Shirika la Bima hiyo iliyopo katika Halmashauri Manispaa ya Morogoro.
Mgeni rasmi (wa pili kulia) Ndg. Kusaya akikabidhi Kitabu cha mwongozo wa Bima ya Mazao kwa Mkulima mmoja aliyehudhuria hafla hiyo, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Bima ya Mazao Tanzania (NIC) Dkt. Doriye
Katika hafla hiyo Ndg. Kusaya amewashauri wakulima katika Mikoa yote hapa nchini kutembelea NIC ili kupata huduma ya bima ya kilimo ambayo itawakinga na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo mlipuko wa magonjwa wa mimea, visumbufu, ukungu, mafuriko na ukame.
Aidha, katika tukio hilo Ndg. Kusaya amekabidhi hundi ya Shilingi Mil. 23,000,000/= kwa wakulima hao watano kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ikiwa ni fidia ya hasara waliyoipata katika mashamba yao yaliyoathiriwa na mafuriko na visumbufu hali iliyopelekea wakulima hao kupata mavuno pungufu.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na utoaji wa huduma za kuendeleza biashara (TAPBDS) Nyakainja Manyama (wa pili Kulia) ambaye amehudhuria hapo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo.
Katika hatua nyingine Ndg. Kusaya ametoa wito kwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika NIC Kutanua wigo wa kutoa huduma zao ili kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini kutokana na fursa iliyotolewa na Mhe. Dkt .John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuondoa tozo zisizo za lazima katika bidhaa za Bima ya mazao.
Akizungumzia lengo la kuanzishwa mfuko wa shirika la Bima ya mazao Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Dkt. Elirehema Doriye, amesema ni kuwawezesha wakulima kukabiliana na majanga yanayoisumbua sekta ya kilimo kwa muda mrefu Tanzania.
Mgeni rasmi (wa kwanza kushoto) akiwakabidhi wakulima watano Hundi ya Mil. 23,000,000/= ikiwa ni sehemu ya fidia ya mazao yaliyo haribikia shambani.
Dkt. Doriye ametaja mafanikio amabayo yametokana na kuanzishwa kwa huduma ya Bima hiyo kuwa zaidi ya wakulima 562 wamejiunga katika huduma ya Bima ya mazao ambapo idadi hiyo inajumuisha wakulima wa Pamba, Mpunga, Mahindi na Pareto.
Dkt. Dorinye ametaja mafanikio mengine ikiwa ni pamoja na wakulima zaidi ya 10,716 kutoka Mikoa ya Simiyu, Morogoro, Njombe na Iringa wameweza kupata Elimu ya Bima, faida zake na jinsi inavyofanya kazi.
Mkuu wa Kitengo cha Afisa Mahusiano NIC Karimu Meshacki akitoa shukrani kwa Katibu Mkuu mara baada ya hutuba yake.
Licha ya mafanikio hayo, Dkt Dorinye ametaja moja ya changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni wakulima wengi kutokuwa na imani juu ya huduma ya Bima ya mazao hivyo kufikiria kutopata fidia ikiwa watapata hasara katika mazao yao.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na utoaji wa huduma za kuendeleza biashara (TAPBDS) Nyakainja Manyama, amesema taasisi yake inasimamia ubunifu unaoongeza hamasa ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuweka bidhaa ya mazao ya bima katika mtindo wa vocha inayouzwa shilingi 5,000/=.
Mgeni rasmi akiwa katika Picha ya pamoja na wanufaika wa fidia ya mazao yaliyoharibikia shambani.
Manyama amesema ili Mkulima aweze kukatia bima shamba la ekari moja atahitajika kununua vocha kumi zenye thamani ya shilingi 50,000/= huku akipata kinga yenye thamani ya shilingi 500,000/=
“Mtindo huu wa vocha ni ubunifu uliolenga kuwawezesha wakulima kujinunulia bima taratibu kabla ya msimu wa kilimo na pengine unapofika msimu awe amekamilisha kadi zote kumi” amesema Manyama.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake ambao wamepata fidia ya mazao yao, Mwenyekiti Msaidizi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kanda ya Mvomero Dorica Mlacha, ametoa shukrani kwa shirika la Bima la Taifa kupitia bima ya mazao kwa kuwaaminisha wakulima kuwalipa fidia ya mazao yanayoharibika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Baadhi Wafanyakazi wa Shirika la Bima ya mazao waliohudhuria katika hafla hiyo.
Shirika la Bima ya mazao la Taifa (NIC) lina uzoefu wa Miaka 57 katika kutoa huduma nchini. Lilianzisha Bima ya mazao Agosti 2019 ikiwa ina lengo la kuwawezesha wakulima kukabiliana na majanga yanayoisumbua sekta ya kilimo kwa muda mrefu hapa nchini.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.