Baraza jipya la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro limetakiwa kufuatilia Shilingi Mil. 137 zinazotokana na asilimia kumi za mapato ya ndani ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ili pesa hizo zirudi kuwafaidisha wananchi wengine.
Hayo yamebainishwa Disemba 15 Mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa kikao cha kwanza cha baraza la Madiwani kilichofanyika katika Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akihutubia Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro.
Akiwa Mgeni rasmi katika kikao hicho, Loata amesema Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga imeshindwa kujibu hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi wa pesa za Serikali (CAG) juu ya upotevu wa shilingi Mil.137 zinazotokana na asilimia kumi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Aidha, Loata amewataka Madiwani kutojihusisha na ukusanyaji wa pesa za mapato ya ndani bali wasimamie katika upatikanaji wa mapato hayo ili kuleta miradi ya maendeleo kwa wananchi wao.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga wakiwa makini kumsikiliza Mkuu wa Mkoa akiwa anawahutubia.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mteule wa baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Edison William amesema atalifanyia uchunguzi agizo la Mkuu wa Mkoa huyo ili kubaini watendaji ambao wametumia vibaya pesa hizo na kuhakikisha zinarejeshwa ili ziweze kuwanufaisha walengwa
Akizungumzia suala la uwepo wa vikundi hewa ambavyo inasemekana kunufaika na asilimia kumi za mapato ya ndani, William amesema atahakikisha anaunda baraza maalumu la kusimamia vikundi hivyo lengo likiwa ni kuwafikia walengwa wa fedha hizo kwa mujibu wa sheria inavyowataka.
Mwenyekiti Mteule wa baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Edison William akitoa nasaha kwa Madiwani wenzake
Naye, Diwani wa Kata ya Lupingu Amina seif, amesema katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) atahakikisha anawasimamia vyema asilimia hizo kumi za Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu hivyo kuwataka kutokuwa na hofu
Hata hivyo, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Fabian Likoko amesema mpaka sasa wameweza kupunguza deni kutoka Mil. 137 nadi Mil. 66 ambapo jitihada zinaendelea kufanyika kwa vikundi ambavyo havijarejesha ili viweze kurejesha pesa hizo kwa wakati.
Maafisa Kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Idara ya Serikali za Mitaa, walishiriki Kikao cha Madiwani katika kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Viongozi wa Baraza hilo unafuata Sheria,Taratibu na kanuni. kutoka Kulia ni Christer Njovu na Marcelin Ndimbwa
Pia, Likoko amesema Idadi ya Vikundi ambavyo vimesajiriwa tangu mwaka 2011 ni 1,027, ambapo mwaka wa fedha 2018/2019 na 2020/20021 jumla ya vikundi ambavyo vimekopeshwa ni 169 na kupewa jumla ya shshilingi Mill 388.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.