Imeelezwa kuwa mpango wa unywaji wa maziwa ya soya mashuleni ulioazishwa Mkoani Morogoro, unakwenda kupunguza utoro mashuleni na kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa kuwa wanafunzi watapata lishe bora kwa wakati na kutumia muda mwingi kusoma.
Hayo yamebainishwa Julai 14, 2025, na Alhaji Adam Kighoma Malima Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati akizindua mpango wa unywaji wa maziwa ya soya katika viwanja vya Shule ya Msingi Juhudi iliyopo Kijiji cha Mtego wa Simba, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mkoani humo.
Mhe. Malima amesema, ukosefu wa lishe bora kwa watoto mashuleni ni chanzo kikubwa cha kushuka kwa kiwango cha uelewa na ufaulu kwa wanafunzi, hivyo jitihada za uanzishwaji wa programu hiyo ya maziwa ya soya zitaenda kupunguza ama kuondoa kabisa changamoto hiyo kwa wanafunzi.
“...Mtoto anaweza kushinda asubuhi mpaka jioni bila kupata chochote. Sasa hali hiyo inaathiri mchango wake shuleni, lakini pia inaathiri matokeo yake, afya yake, na lishe yake,” amesema Adam Malima.
Aidha, Malima ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuhakikisha kuwa kijiji cha Mtego wa simba kinaendelezwa kuwa kitovu cha uzalishaji wa zao la soya ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa malighafi hiyo muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa ya soya kwa ajili ya wanafunzi.
Akieleza faida ya zao la soya, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, karibu nusu ya watu wa China wanatumia maziwa ya soya, hivyo amewataka wananchi wa kijiji cha mtego wa simba na wana Morogoro kwa ujumla kujikita katika kilimo cha zao hilo ili kuinua uchumi wao kwa kuwa soko lake linapatikana nchini humo na sehemu nyingine ulimwenguni.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa Adam Kighoma Malima ameahidi kutoa shilingi milioni moja kwa ajili ya kituo kinachozalisha maziwa ya soya cha Mtego wa Simba kwa lengo la kuzalisha maziwa ya kunywa kwa wanafunzi 350 kwa siku tano ambazo zitapewa jina la ADAM MALIMA SOYA MILK DAYS ili wanafunzi kujizoesha kunywa maziwa hayo kabla ya kuanza rasmi program ya miaka mitatu ya kunywa maziwa hayo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rozalia Rwegasira, amesema mradi huo wa lishe ya maziwa ya soya unaofadhiriwa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China utaongeza afya bora kwa wanafunzi, utaongeza mahudhurio, kupunguza utoro mashuleni na kukuza soko la soya.
Naye Prof. Li Xiayuan kutoka China ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia viongozi wa Serikali ngazi ya Mkoa kwa kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha programu hiyo inafikia malengo ya kusaidia wanafunzi kupata lishe bora mashuleni.
Bi. Nuru Kunugani, kwa niaba ya wakazi wenzake wa Kijiji cha Mtego wa Simba, amepongeza hatua hiyo ya uanzishaji maziwa ya soya kwamba kwa muda mrefu watoto wao walikuwa na changamoto ya kutopata lishe mashuleni na kushindwa kufanya vizuri darasani na kubainisha kuwa kwa sasa wana matumaini ya watoto wao watapunguza utoro na wataongeza ufaulu wa mitihani yao.
Programu ya unywaji wa maziwa ya soya katika Shule ya Msingi Juhudi, inatarajiwa kutekelezwa katika shule mbalimbali mkoani Morogoro kama sehemu ya juhudi za Serikali ya awqmu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu na wadau wengine wa elimu kuhakikisha mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora katika mazingira rafiki.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.