Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wananwake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii hapa Nchini kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawaezesha wanawake kiuchumi hasa walioko Kijijini ili kujikwamaua kiuchumi.
Waziri Gwajima ameyasema hayo Oktoba 15 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya mwanamke anayeishi kijijini ambayo kitaifa yamefanyika Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro katika Kata ya Mang’ula.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wananwake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akitembelea mabanda ya maonesho ya bidhaa za mikono zinazozalishwa na wanawake.
Dkt. Gwajima amefafanua kuwa endapo mwanamke atajikwamua kiuchumi kupitia majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi, atajiamini na kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi hivyo kuondokana na changamoto zinazomkabili ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia, mila kandamizi na ndoa za utotoni ambavyo vyote kwa kiasi kikubwa vichagizwa na na umaskini.
Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wananwake na Makundi Maalum akisalimiana na viongozi mbalimbali baada ya kuwasili katika Maadhimisho ya siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini.
Kwa muktadha huo, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuimarisha majukwaa hayo kuanzia ngazi ya Vijiji, Kata, Wilaya na Mkoa ili kila mwananke apate fursa ya kujikwamua kiuchumi
“Majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi yaanzie Mtaa, Kata, Halmashauri Mkoa ndio yaje Taifa,Taifa liko jukwaa moja tu lakini vijijini na kwenye mitaa yako Mengi tunataka yasimame imara” ameagiza Dkt. Dorothy Gwajima.
Amesema, yeye mwenyewe atafanya ziara kila ngazi kwa lengo la kutaka kuyaona majukwaa hayo na kuhakikisha yako hai lengo ni kuendelea kupunguza umaskini wa chakula kama takwimu zinavyoonesha kuwa umaskini unashuka kutoka 10% 2015 hadi 8% mwaka 2020.
Aidha amesema kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa na kwa mujibu wa REPOA umaskini unakadiriwa kushuka 0.21% kwa kila mwaka hali inayoonesha kuwa Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuwekeza katika kupunguza hali ya Umaskini hapa nchini.
Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wananwake na Makundi Maalum akizungumza na wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini.
Maadhimisho hayo ambayo yalikuwa na kaulimbiu “Mwanamke Aishiye Kijijini ni Mzalishaji Mkuu wa Chakula; Tumuwezeshe” yana lengo la kutambua mchango wa mwanamke anayeishi kijijini katika kilimo, uhakika wa chakula, kuinua uchumi wa Kaya na Taifa kwa ujumla.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.