Halmashauri ya Mji Ifakara Mkoani Morogoro imetakiwa kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikari (CAG) kwa mwaka 2018/2019 juu ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri kutokamilika bila sababu.
Hayo yamebainishwa Disemba 14 Mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa Kikao cha kwanza cha baraza la Madiwani kilichofanyika katika Halmashauri hiyo.
Akifafanua zaidi, Sanare amesema katika hoja 26 zilizoibuliwa na CAG, Halmashauri ya Mji wa Ifakara imejibu hoja 22 huku hoja 4 zikishindikana kupatiwa majibu, ambapo moja kati ya hoja hizo inahusu zaidi ya Shilingi Bil. 7 zilizotolewa na Serikali kushindwa kukamilisha ujenzi wa jengo la Halmashauri hiyo hadi sasa bila sababu ya msingi.
Aidha, Loata Sanare ametaja hoja nyingine ambayo bado haijajibiwa ni pamoja na zaidi ya Shilingi Mil. 200 kulipwa nje ya mfumo wa ulipaji mapato ya Serikali badala yake fedha hizo zililipwa kinyume na maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
Pia, Loata ameongezea hoja nyingine ya CAG ambayo haikupatiwa majibu ni ukusanyaji wa fedhaa kutoka kwa wananchi bila kuingizwa katika mapato ya ndani ya Halmashauri huku takwimu zikionesha zaidi ya Mil. 200 zilizokusanywa zilitumiwa na watu binafsi kwa maslahi yao.
Kutokana na hoja hizo, Loata Ole Sanare amelitaka baraza jipya la Madiwani la Mji wa Ifakara kufanya kazi kwa kutanguliza maslahi ya wananchi, kuwa na vikao kila baada ya miezi mitatu kujadili hoja mbalimbali na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenyekiti wa muda wa Baraza la kwanza la Madiwani ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero Adam Bibagamba akiongoza kikao hicho
Sambamba na hayo, Loata amelitaka baraza hilo la Madiwani kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati huku akiwasisitiza madiwani hao kulinda fedha zinazotolewa na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopo katika maeneo yao.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Ifakara Abubakari Asenga amewasisitiza Madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wananchi, watendaji wa vijiji, watendaji wa Kata, Wakuu wa idara na wataalamu wengine ili kufikia lengo la kumletea maendeleo mwananchi mmoja mmoja.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero ambaye alikuwa mwenyekiti wa muda wa kikao cha Baraza hilo Adam Bibagamba amelitaka baraza la Madiwani hao kufanya kazi kwa mujibu wa miongozo waliyopewa bila kuangalia changamoto ya mtu mmoja mmoja, Chama au migogoro binafsi.
Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la madiwani katika Mji wa Ifakara Kassim Nakapala ametumia fursa hiyo kuwashukuru Madiwani wote kwa kumthibitisha kuwa mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amewaomba madiwani wenzake kutekeleza wajibu wao katika kuwatumikia wananchi kulingana na ahadi walizozito wakati wa kampeni.
Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro Crister Njovu (kushoto) na Marcelin Ndimbwa wakijadili jambo wakati wa Kikao hicho
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.