Katibu Mkuu TAMISEMI atoa maagizo kwa Maafisa Elimu Nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Adolf Ndunguru amewaagiza Maafisa elimu wote wa Mikoa na Halmashauri hapa Nchini kukamilisha ujenzi wa miradi ya Elimu inayotekelezwa katika maeneo yao kabla au ifikapo Januari 15, mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo ametoa maqgizo hayo Januari 4, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala wasaidizi Idara ya Elimu pamoja na Maafisa Elimu wa Halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Glonency iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Kikao kazi hicho kilichokuwa na kauli mbiu isemayo, uwajibikaji wenye ubora ubunifu na uadilifu ni msingi muhimu katika kuboresha elimu msingi na sekondari Nchini kinalenga kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya mwaka 2024, ili kuweza kusimamia masuala ya elimu na kupata mafanikio.
Aidha, Aldof Ndunguru amewataka Maafisa hao kusimamia kikamilifu ufundishaji na ujifunzaji mashuleni na kuhakikisha walimu wasiotimiza wajibu wao kuchukuliwa hatua stahiki, pia kuhakikisha wanafunzi wote wa darasa la tatu na kidato cha kwanza wanamudu stadi ya lugha ya kingereza ifikapo mwishoni mwa mwaka.
“….. Hakikisheni miradi yote inayotekelezwa kwenye maeneo yenu ya usimamizi inakamilika kabla au ifikapo januari, 15 2024...” amesema Adolf Ndunguru.
Pia Ndungulu amesema chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan tunashuhudia uwezeshaji mkubwa wa rasilimali fedha katika sekta ya Elimu hapa Nchini kwa kugharamia elimu msingi bila ada ya shilingi bilioni 33.3 kila mwezi na kupanua wigo wake hadi kufika kidato cha sita.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2020-2021 hadi 2023-2024 serikali imetoa trilioni 1.41 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za awali msingi na sekondari, ambapo fedha hizo zimejenga shule mpya 380 vyumba vya madarasa 8964, mabweni 46, matundu ya choo 25688, nyumba za walimu 857, ujenzi wa mabwalo 6 na ukarabati wa shule za vituo vya walimu 396 wa elimu ya awali na msingi.
Katika hatua nyingine akibainisha kwa upande wa rasilimali watu amesema jumla ya walimu 28179 wameajiriwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020-2021 na 2022-2023 wakiwemo walimu 16542 wa shule za awali na msingi na walimu 11637 wa shule za sekondari.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Charles Msonde amewapongeza walimu kwa kusimamia vizuri elimu ya awali na msingi hivyo kupelekea wanafunzi wa darasa la kwanza kuweza kusoma, kuandika na kuhesabu.
Amebainisha kuwa hadi kufikia septemba 30 mwaka jana ongezeko lilifikia asilimia 97% ya wanafunzi wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu pia kwa darasa la tatu kutoka asilimia 35% hadi kufikia asilimia 75% kwa wanafunzi wanaojua kuongea lugha ya kingereza.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.