Waziri Ummy apongeza uongozi Morogoro upangaji “Wamachinga”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu ameupongeza Uongozi wa Mkoa Morogoro kuwa Mkoa wa kwanza kutekeleza agizo la Mhe. samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuhakikisha wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga wanapangwa na kufanya biashara zao katika maeneo yaliyo rasmi na salama.
Waziri Ummy Mwalimu ametoa pongezi hizo Septemba 21 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa mpango wa kuwapanga wafanyabiashara ndogo ndogo 788 wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuwapatia vibanda vya kufanyia biashara zao katika eneo la Soko Kuu la Chifu Kingalu lililopo katika Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (kushoto) akimpokea Waziri wa Nchi OR - TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu
Amesema mafanikio ya kutekeleza agizo la Mhe. Samia Suluhu Hassan alilolitoa Juni 15 mwaka huu la kutaka wamachinga kutafutiwa maeneo rasmi ya kufanyia biashara, yanatokana na uongozi Mzuri wa Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela kwa kupenda kulea, kuwaamini na kuwashirikisha viongozi waliochini yake masuala ya kimaendeleo huku akimtaka Mkuu huyo wa Mkoa kuendelea na utamaduni huo.
“shigela ni Mkuu wa Mkoa anaependa kushirikisha na kuwaamini waliochini yake….. kipekee na mimi nipongeze sana viongozi wa Mkoa wa Morogoro chini ya Jemedali Martine Shigela kwa kuongoza vyema na kusimamia vyema jambo hili” amesema Ummy Mwalimu.
Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya morogoro Albert Msando (wa pili kulia)na baadhi ya viongozi wa Wilaya hiyo.
Aidha, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando kwa uthubutu, ubunifu na kujitoa kwake kuhakikisha kwamba maagizo ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan yanatekelezwa kwa wakati.
“Hongera sana Mkuu wa Wilaya kwa kuanza vizuri ninaamini Wakuu wa Wilaya wengine watajifunza kutoka kwako, ukipewa nafasi acha alama katika kuwatumikia wananchi hususan wanyonge” aliongeza Waziri Ummy.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya wakimpokea Waziri
Waziri Ummy amesema lengo mahususi la kutatua kero za wamachinga ni kutaka kujenga uchumi imara unaoakisi hali halisi ya Mtanazania kwa kujenga viwanda vidogo na biashara ndogo ili kukuza pato la Taifa, hii pia ni utekelezaji wa ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2020/2025.
Ameongeza kuwa takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa wafanya biashara ndogo ndogo wanaajiri watanzania takriban milioni 31 kati ya watanzania takriban milioni 60 waliopo hapa nchini hivyo Wamachinga ni sehemu muhimu ya kuifanya Tanzania isonge mbele kiuchumi.
baadhi ya mitaa ya maeneo ya kufanyia biashara wamachinga inavyoonekana
Kwa sababu hiyo, Ummy Mwalimu ameziagiza Halmashauri zote hapa nchini, kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo na kuyaendeleza maeneo hayo kulingana na wakati na idadi ya wamachinga inavyoongezeka katika eneo husika huku akitaka mikoa mingine kujifunza Mkoa wa Morogoro jinsi ulivyotekeleza agizo hilo.
Baadhi ya Wafanyabiashara ndogo ndogo (wamachinga) walioshiriki kwenye uzinduzi huo, kulia ni sehemu ya jengo la Soko Kuu la Chifu Kingalu
Sambamba na agizo hilo amezitaka halmashauri hizo kutatua changamoto za Wamachinga za kutosajiri biashara au huduma wanazotoa ili kuwafikia kiurahisi lakini pia wao kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali huku akiagiza Uongozi wa Mkoa na Halmashauri zake kutoa mikopo isiyo na masharti magumu kwa wamachinga hao ili dhamira ya kulinyanyua kundi hilo iweze kufikiwa.
Mhe. Ummy Mwalimu Waziri na MB
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo ambaye alishiriki uzinduzi huo pamoja na kuwatambua wamachinga kuwa ni kundi muhimu kwa uchumi wa nchi bado amewataka kuheshimu taratibu wanazokubaliana ili kuendeleza Amani, utulivu na ustawi wa nchi kupitia kazi wanazozifanya katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine Prof. Mkumbo amewataka wamachinga kuwa wazalendo kwa kununua bidhaa za viwanda vidogo vilivyoanzishwa hapa nchini na kuwauzia wananchi bidhaa hizo pamoja na wao wenyewe kuanzisha viwanda vidogo au vidogo sana ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (kulia) mara baada ya kuwasili Soko Kuu la Chifu Kingalu
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela pamoja na kuwapongeza Viongozi wa Halmashauri ya Manispaa na Wilaya ya Morogoro amewataka wamachinga kuungana na kuwa wamoja huku akiwataka wenye tabia ya kuuza kwa watu wengine maeneo waliyopewa kuacha mara moja tabia hiyo na kwamba atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa makubaliano.
Mkuu wa Mkoa Martine Shigela akimuongoza mgeni wake kukagua vibanda vya wamachinga kabla ya kuzindua. Kushoto ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mpango huo wa kuwapanga wamachinga kwenye maeneo rasmi kwa kuwajengea vibanda unatekelezwa kwa awamu awamu, ambapo awamu hii ya kwanza wamachinga wapatao 788 wamejengewa vibanda vya kufanyia biashara zao na awamu zijazo zitaelekezwa sokoni hapo na kwenye masoko mengine yaliyopo ndani ya Halmashauri hiyo.
wa tatu kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini Mhe. Abood Azizi
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.