Hali ya utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano Mkoani Morogoro imeendelea kushuka kutoka asilimia 33.4 hadi asilimia 26.4 mwaka 2018 kutokana na Serikali kutoa msisitizo katika kuzingatia masuala mbalimbali ya lishe kwa watoto wadogo, Mama wajawazito na walio katika umri wa kuzaa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akiteta neno na Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro mara baada ya kufungua kikao.
Hayo yamebainishwa na Afisa lishe Mkoa wa Morogoro Bi.Salome Magembe wakati wa kikao cha tathmini ya nusu mwaka ya utekelezaji wa mkataba wa lishe pamoja na Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF) kilichofanyika Februari 3, mwaka huu katika ukumbi wa jengo la NSSF katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Bi. Salome amesema hali ya watoto wenye utapiamlo inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na elimu inayotolewa kupitia kwa wahudumu wa Afya ngazi ya vijiji ambapo kila kijiji kina wahudumu wa Afya wawili waliojengewa uwezo wa kutoa elimu kwa akina mama na jamii kwa ujumla.
Aidha, Bi. Salome amebainisha kuwa hali hiyo ya kushuka kwa utapia mlo mkoani Morogoro, inatokana na utekelezaji wa Mkataba wa Lishe uliosainiwa mwaka 2018 baina ya Wakuu wa Mikoa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya Serikali.
Mratibu wa Lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe akiwasilisha taarifa yake katika kikao cha Tathmini
Akifungua Kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kumtengea Shilingi 1000/= kila mtoto wa umri chini ya miaka mitano kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kuboresha lishe kwa watoto hao.
‘’Hakikisha shilingi 1,000/= ambazo Halmashauri zilielekezwa kutenga katika bajeti kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato ya ndani kwa ajili ya kuboresha lishe ya kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kuhakikisha zinatolewa na kutumika kikamilifu kama inavyotakiwa’’ aliagiza Loata Sanare.
Katika hatua nyingine Loata Sanare amesema, moja ya vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha watanzania wengi wanajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya hususani wanatoka katika sekta zisizo rasmi ili kufikia lengo la kila Mtanzania kuwa na Afya Bora.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ni muhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuhamasishwa kujiunga katika Mfuko wa Bima ya Afya yaani iCHF kwani mfuko huo utamwezesha mwananchi kupata matibabu wakati wowote anapohitaji huduma ya matibabu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akitoa vyeti vya pongezi kwa baadhi ya Halmashauri za Mkoa wa Morogoro zilizofanya vizuri katika kupunguza udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Akiwasilisha taarifa wakati wa kikao hicho, Mratibu wa iCHF Mkoa wa Morogoro Bi. Elisia Mtesigwa amesema Mkoa wa Morogoro umekwisha andikisha kwenye mfuko wa Bima ya Afya kaya 46,000 sawa na asilimia 8 ya kaya 565,000 zinazotakiwa kuandikishwa, huku kaya zinazoweza kupata matibabu (kaya hai) zikiwa ni 20,200 Pekee.
Bi. Elisia amesema, endapo Mkoa utatekeleza agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI Selemani Jafo (MB) la kutaka kila Mkoa uandikishe angalau 25% ya idadi ya kaya zilizoko katika Mkoa husika kwenye mfuko wa iCHF, Mkoa utakusanya shilingi 4.4 Bil. na kufanya Mkoa kuwa na uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Afya ambapo itasaidia kulipa zaidi ya shilingi 350 mil. kwa mwezi kwa kila kituo cha kutolea huduma za Afya.
Mratibu wa CHF Mkoa wa Morogoro Bi, Elisia Mtesigwa akiwasilisha taarifa mbele ya Kikao hicho
Hata hivyo, Bi. Elisia Mtesigwa ametaja changamoto zinazokwamisha zoezi hilo kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kutojua faida ya kujiunga na Mfuko wa iCHF na waliokwishajiunga kushindwa kuhuisha kadi zao muda wake unapokuwa umekwisha.
Baadhi ya Viongozi kutoka katika Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Morogoro wakiwemo Wakurugenzi Watendaji na Wakuu wa Wilaya waliohudhuria katika kikao hicho cha tathmini ya nusu mwaka ya utekelezaji wa mkataba wa lishe pamoja na Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF)
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akimkaribisha Mkuu wa Mkoa huo kufungua kikao hicho, aliwaeleza wajumbe wa kikao kuwa tathmini ya Mkataba huo ni ya tatu tangu ilipoanza mwaka 2018 na ina lengo la kujipima malengo waliojiwekea kama yanafikiwa ili kutekeleza mkataba wa Lishe waliosaini Wakuu wa Mikoa.
Aidha, Mhandisi Kalobelo amesema pamoja na maendeleo yaliyopo ya kupunguza udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano, bado jitihada zaidi zinahitajika kwa watendaji wote wa Serikali mkoani humo husuan wa Sekta ya Afya ili kutekeleza kwa asilimia mia mkataba uliosainiwa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akiongea na wajumbe wa kikao hicho muda mfupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa huo Loata Ole Sanare kufungua kikao hicho
Baadhi ya wataalam kutoka sekretarieti ya Mkoa waliohudhudhuria katika kikao hicho, wakwanza ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Dr Rozalia Rwegasira, katikati ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Herman Tesha, wa tatu ni Rhobin Deus Afisa Tehama Msaidizi.
Hata hivyo, ametaka uhamasishaji kwa wananchi Mkoani Morogoro juu ya kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya CHF, ufanyike kwa ushawishi wa kueleza faida za mfuko huo na sio kwa kulazimisha.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro waliofanya vizuri katika kupunguza udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.