Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewasilisha ombi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto la kuomba kuongezewa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Mkoa huo kwa kuwa waliopo hawatoshi ukilinganisha na uhitaji na migogoro iliyopo.
Mhandisi Kalobelo ametoa Ombi hilo Novemba 9 mwaka huu Ofisini kwake mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ambaye yupo Mkoani hapa kikazi.
Akiwa na mgeni wake ofisini, wawili hao walizungumzia umuhimu wa Maafisa wa Ustawi wa Jamii, huku Mhandisi Kalobelo akitoa ombi maalum kwa Dkt. Jingu kuona namna ya kuongeza Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoani humo ili kutatua changamoto na kero ambazo pamoja na kuzipunguza bado zipo kwa kiwango kikubwa.Mhandisi Kalobelo amesema kuna upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii hali inayopelekea mrundikano wa wananchi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, amemuomba Katibu Mkuu huyo kumuongezea Maafisa Ustawi wa Jamii ili wasaidie katika kupunguza mrundikano wa kero Mkoani humo.
“Ustawi wa Jamii wapo wachache hilo ndilo ombi langu pia katika sekta yako tusaidie, tuombee tupate Maafisa Jamii wa kutosha kwa sababu tunatumia gharama kubwa sana” Alisema Kalobelo.
Kwa upande wake Dkt. John Jingu amekiri kuwepo kwa upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii ambapo amesema kwa sasa wamewasilisha taarifa TAMISEMI juu ya hitaji hilo na wameandaa muundo wa kuwaajiri Maafisa Ustawi wa Jamii katika Kada mbalimbali katika Ofisi za Serikali.
Aidha, Dkt. Jingu amesema Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii ni Kada muhimu ambazo huwa za kwanza kupelekwa kwenye maeneo ya majanga ili kuiweka jamii husika katika hali ya utulivu kwa kuwa Kada hizo ndizo zinajua namna ya kufanya kazi na jamii iliyopatwa na majanga.
Akihakikisha dhana hiyo Dkt. Jingu amesema mafisa hao ndio waliosaidia sana wakati wa tukio la Moto lililotokea Mkoani Morogoro Agosti 10, 2019 na kusababisabisha zaidi ya watu 115 kupoteza maisha.
Hata hivyo, Dkt. Jingu ameonekana kupokea Ombi la Katibu Tawala wa Mkoa huo, huku akiwahakikishia wananchi kuwa kada hiyo imezungumzwa sana kwenye ilani ya sasa ya chama kilichoko madarakani hivyo wanaendelea kuiboresha kulingana na maelekezo ya Ilani hiyo ili maafisa hao waweze kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Kwa mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mororgoro Bi. Jesca Kagunila amesema Mkoa wa morogoro una jumla ya Maafisa Ustawi wa Jamii 34 tu sawa na asilimia 10.4.
Aidha Mkoa huo una upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii zaidi ya 282 jambo ambalo amesema linakwamisha ufanisi wa kutekeleza majukumu ya kada hiyo ndani ya Mkoa wa Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.