Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amelipongeza jeshi la polisi hapa nchini kwa kazi nzuri inayoendelea kufanywa na jeshi hilo, kwa weledi mkubwa na kasi inayotakiwa katika kuwalinda watanzania na mali zao.
Mkuu wa Mkoa mhe, Adam Malima amesema kwa sehemu kubwa jeshi hilo limekuwa likitupiwa lawama nyinngi kuhusu utendaji wake wa kazi kubadilika na kuwa na mtazamo chanya kwa jeshi hilo kwa kuwa linakabiliana na uhalifu kila kukicha hivyo watanzania hawana budi kulishukuru.
Mkuu wa Mkoa huyo amebainisha hayo Novemba 27, mwaka huu kutokana na kukamatwa kwa Seleman Mabura Sita mtuhumiwa wa mauaji ya Mama na Mtoto yaliyotokea kata ya Milola Wilaya ya Ulanga Mkoani humo Novemba 24, mwaka huu kwa kuwakata vichwa na kutokomea navyo kusikojulikana.
Hata hivyo, jeshi hilo la polisi chini ya Uongozi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camilius Wambura mtuhumiwa wa mauaji amekamatwa ndani ya saa 36 na kwa sasa anashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano zaidi.
Kutokana na kazi hiyo kubwa na nzuri iliyofanwa na jeshi hilo kwa kumkamata mtuhumiwa aliyefanya tukio hilo ambalo limeleta simanzi kwa jamii, Mkuu wa Mkoa huyo amempongeza IGP. Camilius Wambura, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Alex Mukama na Watendaji wake pamoja na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kwakuendelea kutekeleza vema majukumu yao.
Aidha, Mhe. Malima amesema kuwa ukatili kwa jamii ni jambo lisilokubalika na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutoa taarifa mapema kwa vyombo hivyo ili kufanya kazi haraka na kwa weledi.
"...sisi hatutokaa tukayachekea kabisa matukio haya na niwahakikishie wanamorogoro waendelee kushirikiana na kuwa na Imani na vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yao lakini hata serikali ya awamu ya sita haikubaliani na matukio ya ukatili kama huu..."
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vifaa muhimu vyenye teknolojia ya kisasa sambamba na magari, vitendea kazi ndivyo vilivyosaidia jeshi hilo la polisi kufanya kazi zao haraka na kwa ufanisi.
Pia, Mhe. Adam Malima ametoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na wapendwa wao na kuwataka kuwa wavumilivu na wztulivu wakati jeshi hilo linaendelea kukamilisha taratibu nyingine za kisheria ili haki iweze kutendeka.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.