Mkoa wa Morogoro ulipokea shilingi zaidi ya trilioni tatu (3) kwa kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), fedha ambazo zilielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma malima wakati akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya kikao cha wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Morogoro kilichofanyika katika Ukumbi wa Magadu, Manispaa ya Morogoro.
"...Serikali inaendelea kutekeleza ilani, hadi sasa juni 2025 Mkoa wa Morogoro kwa kutekeleza ibara 14 kwa vyanzo vya fedha 21 jumla ya fedha zilizotambulika kutumika ni zaidi ya Bil.3 ," amesema Mhe. Adam Kighoma Malima.
Mhe. Malima amesema kwa kipindi cha miaka mitano, utekelezaji wa Ilani CCM umeigusa sekta mbalimbali zenye thamani ya shilingi Bil. 618 zikiwemo Utawala, Elimu, Afya, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, uwezeshaji wa kiuchumi, Maendeleo ya ushirika, maliasili na utalii, ardhi, ustawi wa jamii, usafi na mazingira, masoko, michezo na utamaduni pamoja na usafirishaji.
Sambamba na taarifa hiyo, amesema taasisi za umma kwa kipindi cha miaka mitano katika sekta ya miundombinu ya barabara na madaraja zimepokea zaidi ya shilingi bilioni 948.7, sekta ya maji bilioni 422.4, na sekta ya nishati zaidi shilingi trilioni 1.2.
Mhe. Malima amefafanua kuwa sekta ya afya imetumia zaidi ya shilingi bilioni 64.6 kujenga vituo vya afya 33, zahanati 82 na hospitali za wilaya 7. Aidha, fedha hizo zimetumika kununua vifaa tiba pamoja na kuongeza watumishi wa kada ya afya.
Sekta ya elimu imetumia zaidi ya shilingi bilioni 261 kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari 165, vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya kati na vyuo vikuu, pamoja na utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo kwa ngazi ya msingi na sekondari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joseph Masunga ameishukuru Serikali ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuendelea kutekeleza ilani ya chama hicho kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo imewagusa moja kwa moja wananchi na kutatua kero zao.
Kikao hicho kimetoka na maazimio kumi ambayo yalisomwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Ndg. Nuru Ngereja. Baadhi ya maazimio hayo ni pamoja na kuiagiza Serikali ya Mkoa huo kuratibu mashamba yote yanayomilikiwa na watu kwa muda mrefu lakini hayatumiki na kuandaa mpango mkakati wa kurejesha ardhi hiyo kwa wananchi.
Mashamba hayo ni pamoja na shamba la mwekezaji wa zao la karangamiti lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 40,000 lililoko Wilaya ya Ulanga, pamoja na mashamba mengine yaliyoko Wilaya ya Kilosa na Mvomero.
Mazao mbadala na ya kimkakati kama vile tumbaku, michikichi, kakao, viazi mviringo, parachichi na mazao ya viungo kama karafuu, yamepewa msisitizo kulimwa mkoani humo kulingana na maeneo yaliyopo na hali ya hewa ya eneo husika.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.