Mgogoro uliokuwa unafukuta kwa muda mrefu baina ya Kata ya Mbuyuni na Kata ya Magadu ya kugombania shule ya Sekondari ya SUA katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo kila upande unadai kuwa shule ya SUA ni mali yao, umetatuliwa kiaina kwa watendaji wa Mitaa kutwishwa mzigo wa kujenga vyumba vitano vya madarasa ndani ya mwezi mmoja.
Uamuzi huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare alipotembelea Kata hizo za Mbuyuni na Magadu na kukuta hakuna dalili zozote za ujenzi wa vyumba vya madarasa sababu kubwa ikiwa ni mvutano uliopo wa nani mmiliki halali wa shule ya Sekondari ya SUA.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili na kujiridhisha kuwa yapo marumbano hayo Mkuu wa Mkoa akatoa maelekezo kuwa mvutano huo hauna tija kwa wananfunzi wanaohitaji kuingia madarasa yanayotakiwa kujengwa haraka ili kuanza masomo yao hivyo akawageukia Watendaji wa Mitaa ya kata zote mbili na kutoa maagizo kwao.
Katika maagizo yake kwa watendaji hao ametoa mwezi mmoja kujenga vyumba vitano vya madarasa pembeni kidogo mwa majengo ya shule hiyo ya SUA lakini ndani ya eneo la shule hiyo ili kukamilisha haraka na hivyo kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Madarasa katika Shule hiyo.
Akibainisha zaidi, Loata Sanare amesema Kata ya Mbuyuni yenye mitaa sita itajenga vyumba viwili vya madarasa na Kata ya Magadu yenye mitaa tisa itajenga vyumba vitatu vya madarasa hivyo kukamilisha vyumba vitano vya madarasa ambapo amewapa mwezi mmoja watendaji hao kukamilisha ujenzi huo na kufikia usawa wa linta kisha kumkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ili kuyamalizia.
Akitoa ushauri wake katika kumaliza mvutano uliokuwepo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka vingozi wa pande zote mbili kukubaliana nae kujenga madarasa hayo matano mbali kidogo na majengo ya sasa ya shule hiyo na yatakapokamilika siku zijazo kupitia majengo hayo wanaweza kuamua kuifanya shule inayojitegemea, hivyo kila kata kuwa na shule yake na kuondoa mvutano uliokuwepo wa kutaka kila mmoja kuwa mmiliki wa shule hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mbuyuni Mhe. Samwel Msuya amebainisha changamoto iliyokuwepo katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya SUA kuwa ni baada ya kata yake ya Mbuyuni kushtakiwa na kukatazwa kuendeleza shule hiyo hali ambayo ilipelekea kudolora kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Msuya amesema hadi sasa changamoto hiyo imekwishatatuliwa na wananchi wa mbuyuni na magadu wapo tayari kuendeleza ujenzi wa madarasa katika Shule hiyo.
Naye Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga amesema, umiliki wa shule hiyo iwe ya nani siyo muhim kwao, kinachotakiwa ni kujenga madarasa ili watoto waliokosa nafasi ya kusoma waingia madarasani na kuanza kusoma, na kwamba wahusika wakuu wa kujenga madarasa hayo ni wenye watoto ambao ni wazazi wanaoishi kata hizo mbili hivyo amewasihi washirikiane kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa la kujenga madarasa hayo matano.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.