Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ametoa ufafanuzi zaidi kwa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Bonde la Mto Kilombero kutofanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya Bonde hilo huku akisisitiza kutothubutu kuvuka mpaka wa mwaka 2017 kuelekea hifadhini na kuwataka waheshimu mpaka huo hadi pale Serikali itakapotoa maelekezo mengine.
Loata Sanare amesema hayo Ofisini kwake mbele ya vyombo vya habari siku mbili baada ya kikao kilichofanyika Disemba 23 mwaka huu katika Mji mdogo wa Ifakara na kushirikisha viongozi mbalimbali kutoka Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero alipotoa maagizo kwa wananchi wa Wilaya kuheshimu mpaka wa 2017 kupokelewa tofauti na au kupotoshwa na baadhi ya viongozi kwa maslahi yao binafsi.
Amesema katika maagizo yake hakuruhusu watu kulima au kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya Bonde hilo bali aliendelea kusisitiza kuheshimu mpaka wa 2017 na baadhi yao kumnukuu tofauti kwamba ameruhusu watu kuingia ndani ya hifadhi hiyo yaani kuvuka mpaka 2017 na kufanya shughuli zao kilimo na ufugaji jambo ambalo si la kweli.
“Nimesema wananchi tuwatendee haki, kuwa huo mpaka wa 2017 huo ndi mwisho wetu wananchi wetu wapewe walime huku (nyuma ya mpaka huo) waweze kuishi, wasivuke ule mpaka na TAWA tuliwaelekeza ule mpaka ndo uwe mpaka wetu, mpaka hapo tutakapokaa na Mawaziri watatuletea ripoti … kwa hiyo narudia kusema tena, nimesema mifugo itoke, nimesema tena wakulima waruhusiwe kulima mpaka mwisho mpaka ule wa 2017 msiingie kwenye eneo lililotengwa” alisisitiza Loata Sanare.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.