Serikali Mkoani Morogoro imetoa wito kwa Mashirika mbalimbali yasiyo ya Kiserikali, kwa ajili ya kutoa Elimu inayolenga kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ili (VVU) ili kupunguza au kutokomeza kabisa ugonjwa wa UKIMWI.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Mhe. Albinus Mugonya Disemba Mosi mwaka huu kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika eneo la Mafiga katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mugonya ambaye kwenye maadhimisho hayo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Loata Ole Sanare amesema, utoaji wa Elimu kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI utasaidia jamii kujikinga vema na maambukizi kwani bado watanzania wengi wanaendelea kupoteza maisha utokana na kukosa elimu hiyo.
Kwa sababu hiyo Albinus Mgonya ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, Makampuni, Taasisi za Kidini, vyama vya kiraia, mtu mmoja mmoja na wadau wengine kushirikiana na Serikali kutokomeza gonjwa hilo hapa nchini.
Mugonya amesema Mkoa wa Morogoro kushirikiana na Wadau unaendelea na jitihada mbali mbali za kupambana na Ukimwi ikiwa ni pamoja na kutoa kinga, tiba, mafunzo na kuweka mazingira wezeshi katika kutekeleza hatua za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Katika jitihada hizo Mugonya amebainisha kuwa Mkoa wa Morogoro una vituo vya kutolea Afya 440 ambapo kati hivyo, vituo vinavyotoa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU ni vituo 90 ambavyo vimeongezwa kutoka vituo 66 vilivyokuwepo mwaka 2019.
Pia ameongeza kuwa katika jitihada za kuzuia maabukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto Mkoa wa Morogoro una Vituo hivyo 350 zikiwa ni juhudi za Mkoa katika kupambana na ugonjwa huo.
Aidha, ametoa maelekezo kwa kila Halmashauri katika Mkoa wa Morogoro kuunda kamati za kudhibiti UKIMWI hususan katika ngazi ya kata na katika ngazi ya Vijiji ambazo zitakuwa na majukumu ya kufanya utafiti wa hali ya maambukizi ya VVU katika maeneo husika, lakini pia kutambua vichocheo vya maambukizi na kuweka mikakati ya kukabiliana nayo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya mipango na uratibu Anza-Amen Ndossa amewataka wakazi wa Morogoro kuvunja ukimya katika familia zao na kuwataka wazazi wawaelimishaje juu ya ugonjwa huo kutokana na ugonjwa huo kutokuwa na tiba.
“Baba vunja ukimya ongea na mtoto wako wa kike, ongea na mtoto wako wa kiume. Mama vunja ukimya ongea na mtoto wako wa kike, ongea na mtoto wako wa kiume. Baba ongea na Mke wako, Mama ongea na Mme wako. Ukimwi upo, Ukimwi unauwa” alisisitiza Ndossa.
Akisoma hutuba Mbele ya Mgeni rasmi Kaimu Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Morogoro Bi. Tumaini Wapalila, amesema uwepo wa Madangulo, Kumbi za Starehe zinazofanya kazi usiku kucha, Ubakaji, ndoa za utotoni, watoto wa mitaani na mimba za utotoni ni moja ya vyanzo vya maambukizi ya VVU na kuiomba serikali iwasasaidie kudhibiti mambo hayo.
Naye Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Dr. Neema Mtaubo amesema kwa Mwaka 2020 Wananchi waliojitokeza kupima Virusi vya Ukimwi ni 153,367, waliogundulika wameathirika ni 11,809 ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inaongoza kwa maambukizi hayo ikifuatiwa na Kilosa.
Sambamba na hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Albinus Mugonya ametumia fursa ya maadhimisho hayo kukabidhi Pikipiki 37 zenye thamani ya Tsh. 88,000,000 kwa Vikundi viwili vya Bodaboda vya Bomsate na Tunaweza kutoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro pesa ambazo zimetokana na asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Siku ya UKIMWI duniani ambayo huadhimishwa Disemba Mosi kila mwaka hulenga jamii kujitathmini katika maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi, ambapo mwaka huu kauli mbiu ilikuwa MSHIKAMANO KITAIFA, TUWAJIBIKE PAMOJA.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.