Serikali nchini imepiga marufuku matumizi ya kamba za plastiki kwa taasisi zote za Serikali na kuagiza kutumika kwa kamba zinazotokana na zao la Mkonge ili kuongeza soko la uhakika kwa wakulima wa Mkonge.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Hussein Bashe kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wakati wa Mkutano wa pili wa wadau wa sekta ya Mkonge uliofanyika Septemba 13 mwaka huu Ilonga Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Naibu Waziri Bashe akiangalia bidhaa zinazotengenezwa kutokana na zao la Mkonge.
Mhe. Bashe amesema sio tu matumizi ya kamba za Plastiki zinachangia kwa asilimia kubwa kupunguza soko la Mkonge lakini pia mifuko hiyo inauzwa pasina kuwa na nembo ya ubora na zinazalishwa na viwanda bubu ambavyo havijasajiriwa na Serikali.
‘’…Naiagiza Wizara ya Kilimo kutoa tamko la kisera kuzuia matumizi ya kamba za plastiki katika kufungashia mazao mbalimbali na taasisi zote za Serikali ni marufuku kutumia kamba za plastiki badala yake watumia kamba za katani ….’’ amesema Bashe.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (wa tatu kulia) akizungumza na baadhi ya Wakuu wa Wilaya wa Mkoa huo kabla ya kuwasili mgeni rasmi katika Mkutano huo
Naibu Waziri Bashe amemwagiza Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania - TARI na Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha wanakuwa na Ofisi ndogo ya zao la Mkonge Wilayani Kilosa na kuazisha kitalu cha uzalishaji miche kwa ajili ya wakulima wa zao hilo waliopo Mkoani Morogoro.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashe ameitaka TARI kuwasaidia wakulima wadogo kutumia mbinu bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu kwa wakulima kumudu utunzaji wa mashamba na kuwapatia mafunzo ya ugani ynayolenga kutumia eneo dogo la shamba litakalotoa mavuno mengi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema Mkoa wa Morogoro umejipanga vizuri kuwasaidia wakulima wa zao la Mkonge kuhakikisha wanafanya block farming, kuainisha mashamba ya Mkonge na kushirikiana na TARI katika kuwasaidia wakulima kuwapa mashine za kusindika zao hilo la Mkonge.
Sambamba na hayo, amewataka wadau na taasisi za fedha na mifuko ya kijamii Mkoani humo ikiwemo NSSF kujipanga kuleta mashine za kusindika Mkonge ili wakulima wasitumie mashine ndogo zilizopo sasa ambazo haziwezi kutoa Mkonge wenye ubora unaohitajika.
Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mkoani Morogoro Denis Londo akieleza suala nzima la zao la Mkonge.
Aidha, Shigela amewatoa hofu wakulima wa zao hilo kuwa watahakikisha wanawathibiti wafugaji wanaolishia mifugo mazao yaliyopo kwenye mashamba yao na kuwaahidi kutatua changamoto ya Tembo wanaovamia mazao ya wakulima.
Wakizungumzia changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika zao la Mkonge akiwemo Mwenyekiti wa wadau wa zao la Mkonge Damian Luhinda amebainisha changamoto anazokumbana nazo kwenye kilimo hicho kuwa ni ukosefu wa mitaji, ushindani wa bidhaa za Plastiki na kuongezeka kwa kodi.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Mkonge Bi. Mariam Nkumbi ameiomba Serikali kuthibiti changamoto ya Tembo wanaovamia mashamba ya wakulima wakiwemo wakulima wa zao la Mkonge ambao kusababisha hasara kubwa kwao jambo linalopelekea wakulima hao kukata tamaa ya kuendelea kulima zao hilo.
Mkutanao wa kwanza wa Wadau wa uhamasishaji wa zao hilo la Mkonge ulifanyika mjini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, huku mkutano wa sasa uliofanyika hapa Kilosa ni mkutano wa pili ambapo Waziri Mkuu amewakilishwa na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.