.Wajumbe wa kamati ya maadili kwa maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa wameazimia kufanya kikao cha pamoja na wajumbe Kamati kama hiyo ngazi ya Wilaya ili waweze kupitia kwa pamoja mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili kwa lengo la kuboresha zaidi utendaji wa Kamati hizo.
Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha Kamati ya Maadili kwa maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa yenye wajumbe saba (7) kilichofanyika leo Februari 9 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Wakiwa katika kikao hicho cha kawaida kwa ajili ya kujadili ajenda mbalimbali ikiwa ni pamoja na malalamiko ambayo yamepokelewa kutoka kwa wananchi kuhusu Utendaji wa mahakama likajitokeza suala la kutakiwa kupitia mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili.
Hilo limejotokeza kutokana na wajumbe wa Kamati hiyo kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia kwenye Kamati hiyo hivyo kulazimika kuutambua vyema mwongozo huo ili iwe rahisi kwao katika kutekeleza majukumu yao.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo ambaye pia ndiye alikuwa Katibu wa kikao hicho alikubaliana na hoja hiyo ya wajumbe na kwamba itatengwa siku ambapo wajumbe wa Kamati ya Maadili ngazi ya Mkoa na wale wa ngazi ya Wilaya kufanya kikao cha pamoja ili kupitishwa kwenye mwongozo huo na mtaalam atakayeandaliwa.
Kwa upande wake Hakimu Mfawidhi Mkazi Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo ya Maadili Abeesira Kalegeya amesema wananchi wanatakiwa kupewa Elimu mahususi kuhusu namna ya kuwasilisha malalamiko yao kwa Kamati ya maadili kwa kuwa wengi wanawasilisha malalamiko yao bila kuwa na ushahidi unaojitosheleza.
Akifunga kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa kamati ya Maadili ya Mkoa amesema kuwepo kikao baina ya wajumbe Kamati ya Maadili ya Mkoa na Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Wilaya itasaidia kupunguza kero mbalimbali za wananchi katika maeneo yao.
Loata Sanare amebainisha kuwa wananchi wamekuwa wakiandika barua za malalamiko dhidi ya mahakama na kuziwasilisha ofisini kwake bila uthibitisho hivyo kupitia kikao watakachokaa pamoja watabaini tatizo na kulifanyia kazi.
Aidha, Loata Sanare ameitaka Kamati ya Maadili ngazi ya Mkoa kufanya kazi zake kwa uaminifu, bidii na weledi katika kuwatumikia wananchi.
“Inaonekana wazi kuwa Kamati hii ina jukumu la kuimarisha uadilifu wa watendaji wa Maafisa wa Mahakama ndani ya Mkoa wetu wa Morogoro hivyo tunalazimika kutekeleza majukumu yetu kwa weledi ya hali ya juu katika kutoa huduma kwa wananchi wetu ndani ya Mkoa’’ amesisitiza Sanare
Kamati ya Maadili ngazi ya Mkoa imeundwa kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji wa Mahakama, sheria Na. 4 ya mwaka 2011, kifungu cha 50 (a) – (c) na kuwataja wajumbe wake kuwa ni Mkuu wa Mkoa (Mwenyekiti), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa husika, Katibu Tawala Mkoa, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa na wajumbe wawili walioteuliwa na Jaji Mfawidhi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.