Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dr. Ashatu Kijaji amewataka wananchi Mkoani Morogoro na watanzania wengine kwa ujumla kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali hapa nchini ili kujiinua kiuchumi na kuchangia pato la Taifa.
Waziri Kijaji ametoa kauli hiyo Mei 14 Mwaka huu katika hotuba yake wakati wa kufunga Maonesho ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi kiuchumi yaliyofanyika Kitaifa uwanja wa Jamhuri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
Dr. Ashatu Kijaji amebainisha kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi zinafanya jitihada kubwa ya kuanzisha Mifuko na Programu mbalimbali za kusaidia na kuwezesha wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi lakini ushiriki wa wananchi wenyewe umekuwa si wa kuridhisha.
“Imetamkwa thamani mbalimbali za fedha ambazo tayari kupitia Programu hizi Serikali imeshatoa fedha kwa Wananchi aidha kupitia mikopo ya moja kwa moja au kupitia mipango mbalimbali ya kutengeneza miundombinu ya msingi kwa ajili ya shughuli zetu sisi wananchi za kiuchumi”. amesema Dkt. Kijaji
“Hatuna sababu ya kurudia lakini tujiulize kama wananchi tunatumiaje fursa hizo? Tupo tayari kuhakikisha na kuona kwamba tunanufaika na jitihada hizi ambazo Serikali yetu ya awamu ya sita imewekeza kwetu”. Amesisitiza Dr. Kijaji.
Katika hatua nyingine, Dr. Ashatu Kijaji amewsihi wananchi na wajasiriamali kuwa, kila mwananchi ajitahidi kwa makusudi na kuitumia vema mikopo kama njia ya kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kwa pamoja taifa litasonga mbele kimaendeleo endelevu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiwasilisha salamu za Mkoa ameweka wazi kuwa, kupitia vikao vya kiutendaji, Mkoa utatumia mikakati mbalimbali na kubainisha Mifuko na Programu za kuwasaidia wananchi kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji hasa katika Sekta ya Kilimo na kukaribisha wawekezaji wa kada hiyo kwani ardhi ipo ya kutosha.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Baraza la Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa amesema tangu kuanzishwa kwake Baraza hilo lina jumla ya Mifuko na Programu 62, kati hiyo 52 inatoka Selrikalini na 10 katika Sekta binafsi, ambapo hadi sasa Mifuko hiyo imeshato Mikopo zaidi ya shilingi trilioni 5.38 kwa zaidi ya wajasiriamali zaidi ya Milioni 8 katika kuimarisha mzunguko wa uchumi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuchochea Kilimo Tanzania Bw. John Kyaruzi amebainisha kuwa Mfuko una lengo la kuwatatulia wakulima wadogo changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo changamoto ya kukidhi viwango vya soko, uhaba wa masoko ya bidhaa, miundombinu isiyo faaa kwa usafirishaji na Mabenki yasiyo na mikopo rafiki.
Changamoto nyingine ni maslahi kwa wakulima na mikataba isiyofaa kwa wakulima hao hali inayopelekea wakulima kuendelea kuwa masikini kila kukicha hivyo taifa nzima kutokuwa endelevu.
MWISHO.
|
|
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.