Jumla ya Wataalamu na watumishi 33 kutoka katika Wilaya ya Kilombero wamehitimu mafunzo ya siku tano yanayolenga kutatua migogoro ya Ardhi ikiwa ni jitihada za Serikali katika kutafuta njia mbadala ya kupunguza kama sio kumaliza kabisa migogoro hiyo Wilayani Kilombero.
Mafunzo hayo yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kilichoko Lushoto Mkoani Tanga na kushirikisha viongozi kutoka Serikalini ngazi ya Mkoa, Wilaya, Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji yalihitimishwa mwishoni mwa wiki hii na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare kwa kutoa vyeti kwa wahitimu wote wa mafunzo hayo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mlimba ulioko katika Mji wa Ifakara.
Kabla ya kugawa vyeti kwa wahitimu hao Mkuu wa Mkoa huyo alisema Mkoa wa Morogoro unakumbwa na changamoto nyingi za ardhi ambapo kupitia mafunzo hayo wahitimu watajengwa uwezo wa kuelewa njia mbalimbali za namna ya kutoa usulihishi kwa kuzingatia ukweli wa kesi zinazowafikia na kuwataka wote waliopata mafunzo hayo kufanya kazi kwa uadilifu na kutoa maamuzi bila upendeleo kwa pande mbili zilizotofautina.
“Ndani ya Mkoa wetu wa Morogoro tuna tatizo kubwa la migogoro ya ardhi karibia kila Wilaya kote mpaka pale Manispaa, achilia mbali hizi wilaya zingine tuna kazi kubwa ya kuhangaika na migogoro ya ardhi ndani ya maeneo yetu” alisema Loata
“…..kwahiyo mlipoamua kutoa mafunzo kwenye Mabaraza haya ni jambo jema kweli, na hasa ukizingatia kuwa kazi ya mabaraza haya ni ya usuluhishi kujua ukweli na kujaribu kusuruhisha, suluhisha kwa kujua ukweli bila kupendelea” alisisitiza Loata.
Katika hatua nyingine Loata Ole Sanare amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo kuomba nafasi za maafisa wawili wa ngazi ya Mkoa kushiriki mafunzo ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi yanayoendeshwa na Chuo hicho cha Uongozi wa Mahakama cha Lushoto Mkoani Tanga.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa huyo amewaagiza Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya Mkoani humo kutenga bajeti kwa ajili ya kusaidia mafunzo ya usuluhishi ambayo yatawashirikisha wafanyakazi kutoka ngazi ya Kijiji hadi Mkoa ili kutambua mbinu za kushughulikia migogoro hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Kilombero SACP Ismail Twahil amesema kutokana na changamoto nyingi zilizopo katika Wilaya hiyo anaamini kupitia mafunzo waliyoyapata washiriki hao watawasaidia wananchi katika kufikia maamuzi ya sahihi katika kutatua migogoro kwa kuzingatia mafunzo waliyoyapata.
Naye, Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Mahakama cha Lushoto Bw. Mlokozi ametoa shukrani kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro, Wilaya wanazotoa mafunzo hayo kwa kuchangia utoaji wa Kumbi kwa ajili ya mafunzo hayo hali ambayo imesaidia pesa ambayo ingetumika kulipia ukumbi kutumika kulipia ushiriki wa mafunzo husika.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Katibu wa Baraza la Usuluhishi wa Kijiji cha Miwangani Masa Nkuba, amesema amenufaika na elimu ambayo ameipata hali itakayosaidia kufanya kazi kwa ufanisi pale ambapo wadau watawaletea kesi za migogoro ya ardhi.
Hata hivyo, ameahidi kumuomba Mwenyekiti wake wa Kijiji kuitisha Mkutano wa hadhara ili kuifikisha kwa wananchi elimu aliyoipata kupitia mafunzo hayo lengo ni kupata urahisi wa kufanya kazi hiyo, lakini pia amewataka wanawake watakao pata nafasi hiyo kuitumia vizuri ili kuelimisha Jamii nzima juu ya namna ya kutatua migogoro katika sehemu zao.
Mafunzo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanafadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani – FAO yanalenga kutoa mafunzo kwa Taasisi za Serikali katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji.
Walengwa wengine ni CSOs zinazohusika na usimamizi wa Maliasili katika ngazi za Vijiji, wasomi katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali za asili na kilimo na jamii, makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi, kamati za amani na makundi ya watu walio katika mazingira hatarishi.
Mafunzo hayo ambayo hadi sasa yamekwishafanyika katika Wilaya ya Mvomero na Kilombero, yanaendelea kutolewa katika Wilaya za Malinyi na Ullanga kuanzia Novemba 30, mwaka huu na lengo ni kuhakikisha yanatolewa kwa Wilaya zote za Mkoa wa Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.