Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kutatua changamoto zinazowakabili vijana kwa kuweka mikakati ya kuboresha miongozo ya stadi za maisha ili kuwawezesha vijana kupata stadi za mahusiano, mawasiliano na ujasiriamali.
Hayo yamebainishwa Agosti 12 mwaka huu na Mkurugenzi wa Hifadhi ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Festo Fute, wakati akifungua kongamano la vijana la Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Edema uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Bw. Fute amesema Serikali imeendelea kufanya mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana, kuanzisha mifuko ya mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana, pamoja na kuongeza nafasi za ajira kila mwaka kupitia bajeti kuu ya Serikali, ambapo vipaumbele hivyo vinakusudia kutatua changamoto zinazowakabili vijana.
“Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika kutafuta ufumbuzi wa masuala yote mlioeleza kwa kuwa yanagusa malengo ya Taifa kuhusu ajira zenye staha,” amesema Fute.
Kwa upande wake, Mratibu wa Vijana THTU Taifa, Bi. Julieth Mchunguzi, amesema lengo la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja vijana kutoka taasisi mbalimbali ili kujadili changamoto na kuweka mikakati ya namna ya kuzitatua changamoto hizo.
Baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana wa elimu ya juu ni pamoja na kutopewa nafasi za kiutawala hata wanapokuwa na sifa na kutopatiwa kipaumbele katika utoaji wa nyumba za watumishi.
Changamoto nyingine ni pamoja na pesa za kujikimu kutotosheleza mahitaji ya waajiriwa wapya, kuwepo kwa ajira za mikataba ya muda mfupi hasa katika taasisi za elimu ya juu, kukosa fursa za kujiendeleza kielimu, kunyimwa likizo za masomo, pamoja na ugumu wa kupata mikopo au kuwepo mikopo yenye masharti magumu.
Naye Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dkt. Paul Loisulie, amesisitiza umuhimu wa kudumisha uhusiano mzuri baina ya taasisi zinazoshirikiana katika kuhakikisha vijana wanaondokana na changamoto walizonazo jambo ambalo litaleta uhai mzuri katika taasisi hizo na kuboresha maslahi ya vijana wa elimu ya juu.
Kongamano hilo lilikuwa na kaulimbiu iliyosema "Vijana katika Maendeleo: Kuimarisha Uvumbuzi kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu"
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.