Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, ametoa siku saba kwa viongozi wa ushirika Mkoani humo kuhakikisha wanaanzisha ........(SACCOS) kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo (machinga), ili kundi hilo liwe rasmi na kuwa na mchango katika maendeleo ya mkoa wa Morogoro na Taifa.
Mhe. Kighoma Malima ametoa agizo hilo Agosti 23, 2025, wakati wa kongamano la wamachinga Mkoa wa Morogoro lililofanyika katika stendi ya zamani ya mabasi madogo ya mjini Manispaa ya Morogoro kongamano lililokuwa kaulimbiu iliyosema: “WAFANYABIASHARA WADOGO WOTE TUJITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU OKTOBA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU.”
Kiongozi huyo wa Serikali amesema, kundi hilo la wafanyabiashara wadogo ni muhimu kulidhamini na kulifanya kuwa kundi rasmi la kiuchumi na kijamii, kwa sababu linachangia pato la halmashauri na taifa kwa jumla.
Aidha, amesema kuazishwa kwa SACCOS hiyo kutasaidia kuwekeza fedha zao na hatimaye kuwawezesha kukopa katika taasisi za kifedha kwa urahisi ili kukuza biashara zao, uchumia wao na wa taifa, hivo akatumia fursa hiyo kutoa maagizo kwq viongozi wa Ushirika wa Mkoa wa Morogoro.
“...Nataka ndani ya siku saba suala la SACCOS la wamachinga lifanyiwe haraka. Ndani ya siku hizo niletewe karatasi nisaini...” amesema Mhe. Adam Kighoma Malima.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi wanaokusanya mapato kutoka kwa wamachinga kutowafungia biashara zao, hatua kama hizo zinaweza kuchukuliwa kwa mhusika endapo hajalipa kodi yake kwa kipindi cha miezi mitatu.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Morogoro, Bw. Gibson Mwakoba, amebainisha kuwa wanyabiashara hao waliosajiliwa kwenye mfumo ni 9,792, ambapo kati yao wanaume ni 3,799 na wanawake 5,993 na walio lipia vitambulisho ni 3,044 na kati yao, wafanyabiashara 2,627 sawa na asilimia 86.3 wamepatiwa vitambulisho.
Naye Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Morogoro, Bw. Faustine Francis Almasi, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kulijali kundi hilo kwa kutoa mikopo mbalimbali inayowasaidia kuinua biashara zao.
Sambamba na hilo, amebainisha changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao, ikiwemo kufungiwa mabanda yao bila makubaliano huku akikiri kuwa changamoto hiyo imeanza kufanyiwa kazi na Mkuu wa Mkoa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.