Wadau mbalimbali wa maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi maarufu kama Nanenane wamewatakia kutekeleza kwa vitendo ujuzi, maarifa na teknolojia mpya walizopata kwa kipindi chote cha maonesho ya Nanenane ili waweze kuongeza tija na thamani ya mazao yatokanayo na sekta hizo.
Agizo hilo limetolewa leo Agosti 8, 2025 na Balozi Dkt. Batilda Burian Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika Viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, vilivyoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
Amesema, wananchi wanapaswa kuyatumia kikamilifu maarifa waliyoyapata wakati wa maonesho, hususan yale yanayohusu teknolojia za kisasa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ili waweze kuongeza kipato chao na kukuza uchumi na pato la Taifa.
“Tuhakikishe tunaishi kile tulichojifunza. Tusiruhusu teknolojia hizi zipite bila kuzitumia,” amesema Mhe. Batilda Burian.
Aidha, amewataka viongozi wa Serikali kutoyachukulia maonesho ya Nanenane mzaha, kwani kufanya hivyo ni kunapoteza malengo msingi ya maonesho hayo badala yake wayatilie mkazo ili yawe chachu ya katika kutoa elimu ya kisasa kwa wananchi, ikiwemo mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema Kanda ya Mashariki inajipanga kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa ya mfano kwa kutekeleza na kusambaza teknolojia zilizowasilishwa katika maeneo mbalimbali ya kanda hiyo ili ziweze kutumika kwa manufaa ya Halmashauri zao.
Aidha, Mhe. Malima amesema katika maonesho hayo kulikuwa na jukwaa la biashara lililojulikana kwa jina la B2B (Business to Business) amesema jukwaa hilo limewakutanisha wataalamu zaidi ya 1,200 wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na taasisi mbalimbali, ambao walipata elimu watakayopeleka maeneo yao kwa lengo la kuongeza thamani katika sekta hizo.
Maonesho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo endelevu ya Kilimo, ufugaji na Uvuvi, 2025" ingawa yamehitimishwa leo, bado yataendelea kufanyika kwa siku mbili ili kutoa nafasi kwa wananchi kuendelea kununua bidhaa mbalimbali ndani ya viwanja hivyo.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.