Wazee wa Kimila wa Mkoa wa Morogoro wamemfanyia tambiko maalum Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kuhakikisha amani, upendo na utulivu vinatawala kuelekea uzinduzi wa kampeni za Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinazotarajiwa kufanyika mkoani humo.
Akizungumza leo Agosti 28, 2025 na wazee wa kimila, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amewashukuru wazee hao kwa kutambua umuhimu wa Kampeni hiyo na kuifanyia tambiko hilo ili kuhakikisha kampeni hizo zinafanyika bila dosari yoyote ndani ya Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.
“Hii ya kwamba mmekuja kufanya dua zenu kufungua njia ili ugeni wa Mhe. Rais upite Morogoro salama, basi mimi nawapongeza na kuwashukuru sana wazee wangu wa Morogoro,” amesema Mhe. Malima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wazee wa kimila Mkoa wa Morogoro, Bw. Angelus Likwembe, amesema ni jukumu lao kuhakikisha wanafanya matambiko hayo ili kudumisha amani na upendo miongoni mwa jamii huku akimhakikishia Dkt. Samia kuwa kutokana na maombi hayo, atakuwa salama Morogoro na kuendelea kuwatumikia wananchi wake.
Naye Afisa Maendeleo ya Michezo na Utamaduni Mkoa wa Morogoro, Bi. Grace Njau, amesema ni wajibu wa kila mwanamorogoro kuhakikisha shughuli za kampeni zinakuwa chanzo cha kupata viongozi bora huku zikidumisha utulivu na kuwataka wananchi kutotumia kampeni hiyo kama fursa ya kuharibu amani iliyopo.
Bi. Njau aliongeza kuwa maombi yaliyofanywa na wazee wa mila katika kudumisha utamaduni wa mwafrika ni ishara kuwa kampeni hizo zitakuwa za amani na utulivu Mkoani humo na taifa kww jumla kwa sababu tayari baraka za wazee zimetolewa.
Ziara ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Morogoro inatarajiwa kuanza Agosti 29 na kuhitimishwa Agosti 30 mwaka huu.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.