Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikuku (kazi Maalum) Captain Mstaafu Mhe. George Mkuchika (MB) ameishukuru na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Mhe. Mkuchika amebainisha hayo Oktoba 27, 2024 wakati akizindua mradi wa maji wa Mangae ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro ya kukagua, kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya Mkoa huo.
Mhe. Mkuchika amesema nia ya Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuendelea kutoa fedha na kutekeleza miradi ya maji hapa nchini ili kumtua mama ndoo kichwani na kuwashukuru watendaji wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi bora wa fedha na kuweza kutekeleza miradi kwa kiwango cha juu.
"...Naishukuru Halmashauri kwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizi hamkuruhusu mchwa kula noti za hapa..." amesema Mhe. George Mkuchika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Mhe. Rais kwa niaba ya wanamorogoro kwa kuwajali na kuwaletea miradi mbalimbali hususan ya maji ambapo hapo awali kipindi cha kiangazi idadi ya mifugo hupungua kwa sababu ya uhaba wa maji ya kutosha ya kunywesha mifugo.
Pia amesema uwekezaji wa ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Mangae utaondoa kero ya upatikanaji wa maji ambapo amemuomba Mhe. Rais kuendelea kutoa fedha katika Mkoa huo ili kuweza kutokomeza adha ya maji.
Naye, Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Mvomero Mhandisi Mlenge Nasib akisoma taarifa ya mradi huo wa maji wa Kijiji hicho amesema mradi huo umegharimu jumla ya shilingi Milioni 643.7 hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi Milioni 388.8 ambapo mradi huo umefikia asilimia 85% kukamilika ambpo utahudumia wakazi 4049 na kuweza kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika kijiji cha Mangae.
Nao wakazi wa kijiji hicho akiwemo Bi. Clinsensia Cosmasi amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwaletea mradi huo wa maji ambapo hapo awali walikuwa wakichota maji kwenye mito hivyo mradi huo pindi utakapokamilika utaenda kuondoa adha walizokuwa wanakumbana nazo kutokana na kutafuta maji.
Ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Mhe. Mkuchika katika Mkoa wa Morogoro ambapo Leo ametembelea miradi mitano iliyopo Wilayani Mvomero hususan ya Afya, Elimu na miundombinu ya Barabara, ambapo Oktoba 28, 2024 kiongozi huyo ataendelea na ziara katika Wilaya ya Gairo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.