Viongozi wa Serikali Mkoani wa Morogoro, wametakiwa kulinda uhai wa Bonde la Mto Kilombero linalochangia asilimia 65 ya maji yote yanayoingia kwenye mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere ili bwawa hilo liwe endelevu.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima Septemba 26, 2025 wakati wa kikao cha pamoja cha kujadili athari zinazolikabili bwawa la umeme la Julius Nyerere baada ya kuona kuwa kuna viashiria vya uharibufu wa vyanzo vya maji hususan mito inayopeleka maji kwenye bwawa hilo.
Akiwa Mwenyekiti wa kikao Mhe. Malima amewataka Wakuu wa Wilaya ambao ni wenye viti wa Kamati za Ulinzi za Wilaya pamoja na Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha ajenda ya kujadili uhai wa Bonde la Mto Kilombero inakuwa ajenda ya lazima katika vikao vyao vyote vya kisheria.
Amesema, jukumu la kulinda vyanzo vya maji vinavyohusisha bwawa hilo ni jukumu la kila mmoja, kwa kuwa bwawa hilo linazalisha megawati 2,115 za umeme na kusisitiza kuwa ni lazima kulinda vyanzo vyake vya maji ili viendelee kudumu na kuliwezesha bwawa kutumika sasa na vizazi vijavyo.
“Suala la uhai wa bonde la kilombero ni la lazima. Naagiza kwamba, katika kila kikao cha Halmashauri, ajenda ya kulinda uhai wa Bonde la Kilombero ni ya lazima na izingatiwe kwa ukamilifu,” amesisitiza Mhe. Malima.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa, endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuzuia uharibifu wa vyanzo hivyo vya maji, baada ya miaka kadhaa bonde hilo litaathirika vibaya na kupoteza uhai wake kutokana na ukosefu wa maji.
Katika hatua nyingine Malima amesema, ili kufanikisha ajenda hiyo ya kulinda bonde hilo, Shirika la Umeme Tanzania -TANESCO lishirikiane na Maafisa Maendeleo ya jamii pamoja na Maafisa Mazingira ngazi ya Wilaya na Mkoa ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu njia bora za kutunza vyanzo vya maji na kuendeleza kilimo hifadhi (kilimo misitu) ambacho hakiharibu mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange, amesema shirika hilo linaendelea kutekeleza mikakati ya kufuatilia na kulinda vyanzo vya maji vinavyopeleka maji katika bwawa hilo huku akikiri kuwepo kwa changamoto za shughuli za kibinadamu katika maeneo yote ya vyanzo vya maji yanayoingia bwawani ndio maana wameanza kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo mapema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la TANESCO, Bi. Irene Gowelle, amesema kikao hicho ni mwanzo tu wa utekelezaji wa yale waliyoyapanga kuyafanya na wana imani matokeo yatakuwa yenye mafanikio kwa sababu kikao hicho kimehusisha wadau wote muhim watakaoshirikiana nao katika kulinda vyanzo vya bwawa hilo la Julius Nyerere.
Ametaja mikakati iliyopo ni pamoja na kuwezesha zoezi la upimaji viwango vya maji vinavyoingia kwenye mabwawa ya umeme, kufukia mifereji isiyo na vibali vya kutumia maji, Kuendelea na upandaji wa miti rafiki kwa maji na Mazingira na kurudisha mito ya maji iliyopoteza mikondo yake.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.