Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amewataka viongozi wanaotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) kuanzisha jarida maalumu litakalohifadhi na kusambaza taarifa za utekelezaji wa programu hiyo na kubainisha mafanikio na changamoto zake.
Dkt. Mussa ametoa ushauri huo leo Septemba 30, 2025 wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua tano kuu za PJT–MMMAM, kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro na kubainisha kuwa jarida hilo litasaidia wananchi kuelewa kwa kina mchango wa programu hiyo katika kuboresha maisha ya watoto.
“Embu tuanzishe Morogoro Journal ya mradi huu, ili kuelezana mafanikio na changamoto” ameshauri Dkt. Mussa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa uandishi wa taarifa na ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa Serikali na wadau wengine wa maendeleo na vingozi kuacha kufanya kazi kwa mazoea bila kushirikiana, jambo linaloweza kudhoofisha kasi ya mafanikio ya programu.
“Ni lazima tushirikiane, tuache kufanya kazi kivyetu. Ushirikiano ndio utakaoleta matokeo chanya na kufanikisha malengo tuliyojiwekea,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Inlighten Development Organization (IDO), Bw. Benito Miwando, amesema Serikali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha utekelezaji wa programu hiyo unafanikiwa na kubainisha kuwa shirika lake limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa malezi bora na makuzi ya watoto, ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa pamoja.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Bi. Joanita Mshasi, amesema halmashauri hiyo imeweka kipaumbele kwenye masuala ya lishe kwa watoto shuleni. Ameeleza kuwa chakula chenye virutubisho sahihi kimekuwa kikitolewa mashuleni ili kuhakikisha watoto wanakua vizuri kiakili na kimwili.
Afua zinazotekelezwa kupitia programu hiyo ni Lishe, Afya, Elimu, Ulinzi na Usalama pamoja na Malezi Yenye Mwitikio.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.