Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro imeendelea na maonesho ya kilimo ambayo hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima na mara hii imejipanga zaidi kuhamasisha kilimo biashara lengo likiwa ni wakulima kuondokana na kilimo chakula ili kuongeza uchumi kwa wakulima.
Hayo yamebainishwa Septemba 24, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa rasmi ya maonesho hayo yanayojulikana kama “Samia Kilimo Biashara Expo 2025" yatakayofanyika wilayani Gairo kuanzia Septemba 28, mwaka huu.
Mhe. Malima amesema Wilaya ya Gairo imekuwa ya mfano katika kutekeleza mapinduzi ya kilimo biashara kwa vitendo, jambo ambalo limeongeza mapato na kuwawezesha wakulima kunufaika moja kwa moja, kwa sababu hiyo, wilaya hiyo imechaguliwa kuendelea kuwa mwenyeji wa maonesho hayo.
" ......katika haya mapinduzi ya kilimo, namba moja ni Gairo...” amesema Mhe. Adam Malima.
Akifafanua zaidi, Mkuu wa Mkoa huyo amesema mkoa pamoja na Wilaya hiyo wamejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuwa kila zao linaweza kuwa zao la biashara endapo tu litazalishwa kwa wingi ama zaidi ya mahitaji ya chakula na hivo kuondokana na kilimo CHAKULA.
Aidha, Maonesho hayo yatakwenda kutoa Elimu ya kilimo biashara hususan matumizi ya mbinu za kisasa za uzalishaji, matumizi ya teknolojia, usindikaji wa mazao, pamoja na kujenga mitandao ya kibiashara.
Katika hatua nyingine Adam Malima amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kuhakikisha Mkoa wa Morogoro unakuwa kinara wa mapinduzi ya kilimo.
Hivyo, ametoa wito kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wote wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo ili wapate elimu ya mbinu bora za kilimo, teknolojia za kisasa na fursa za masoko zitakazoongeza tija na kipato chao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, na kwamba uchaguzi siyo vita bali ni suala la kikatiba katika kuwapata viongozi watakaowaletea wananchi maendeleo yao na kuwataka wanahabari kutumia kalamu zao kuhamasisha uchaguzi huo kuwa wa AMANI, SALAMA na KISTAARABU.
Maonesho ya SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2025 yatazinduliwa Septemba 28, 2025 na kufungwa Oktoba 4 mwaka huu.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.