Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameiagiza serikali wilaya ya Morogoro kufuatilia wanafunzi 82 ambao hawajaripoti katika shule ya Sekondari Majimoto kutokana na sababu mbalimbali na kuwasilisha taarifa hiyo kwenye ofisi yake ndani ya siku nne.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo januari 16, 2024 alipotembelea shule mpya ya Sekondari Majimoto iliyopo Tarafa ya Kisaki katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ikiwa ni muendelezo Wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Mh. Malima ametoa agizo hilo na kumtaka Afisa Tarafa ya Bwakila, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kisaki pamoja na Kijiji cha Kisaki Kituoni kufuatilia wanafunzi 82 ambao hawajaripoti kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2024 katika shule hiyo ni 187 lakini hadi sasa walioripoti ni 105 hivyo amewataka Viongozi hao ngazi ya Tarafa, Kijiji na Kata kufuatilia sababu iliyopekea wanafunzi 82 kutoripoti shuleni hapo.
“...kwanza kuna watoto 82 hawajaripoti naondoka leo kisaki jumanne hadi kufika jumamosi lazima mniambie kwa majina na namba za simu...alafu DC utaniambia umewachukulia hatua gani...” amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mhe. Malima ametoa wiki mbili kwa uongozi wa shule hiyo kukamilisha ujenzi wa vyoo vya wanafunzi pamoja na ujenzi wa maabara hadi kufikia Mwezi Machi mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi hao kufanya utaratibu wa kuwahamisha wanafunzi wanaosoma mbali hususan wa kidato cha Pili na cha Tatu katika shule hiyo ya ya Sekondari Majimoto ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Majimoto Bw. Edmund John amesema wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza 2024 ni 187 lakini hadi sasa wanafunzi walioripoti ni 105, hivyo wanaendelea kufanya jitihada za kubaini Watoto ambao bado hawajaripoti shuleni hapo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.