Askofu Mkuu kiongozi na Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini Mareck Solczynski ameongoza ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Padre Lazarus Msimbe kuwa Askofu mpya wa jimbo katoliki la Morogoro.
Askofu Solczynski ameongoza ibada hiyo Septemba 19 mwaka huu katika viwanja vya seminari ya Mtakatifu Peter jimboni humo iliyohudhuriwa na Maaskofu Wakuu na Maaskofu karibu wote wa Kanisa Katoliki hapa nchini.
Katika mahubiri yake Askofu Mkuu Kiongozi amemtaka Askofu Msimbe kuchunga Kondoo wa Mungu yaani waumini wa Jimbo Katoliki la Morogoro kwa upendo bila kubagua.
Naye Askofu Lazarus Msimbe pamoja na kutoa shukrani zake kwa Viongozi wote wa Kanisa hilo wakiwemo wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki hapa nchini – TEC bado ameiomba Serikali kuendelea kushirikiana katika kuwalea wananchi mahitaji ya kiroho na kimwili.
Mgeni Rasmi katika sherehe hizo alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. George Simbachawene aliyemwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amesema Serikali chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuheshimu mchango unaotolewa na madhehebu ya dini hapa nchini na kwamba itaendele kutoa ushirikiano wa dhati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ambaye aliambatana na Waziri huyo, ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kanisa hilo pamoja na madhebu mengine na katu hatakuwa kikwazo kwao katika shughuli za kutaka kanisa hilo kuwaletea mahitaji ya kijamii kama shule, Hospitali na miradi mingine ya maendeleo.
Padre Lazarus Msimbe amezaliwa 27 Disemba, 1963 amepata Upadre 21 Juni, 1998 na kuteuliwa kuwa msimamizi wa kitume jimbo la Morogoro 13 Februari, 2019 ambapo 15 Mei 2021 aliteuliwa kuwa msimamizi wa jimbo katoliki Askofu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.