Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright amefanya ziara ya siku moja Mkoani Morogoro na kufanya mazungumzo mafupi na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Ofisini kwake.
Balozi Donald Wright amefanya ziara hiyo leo Agosti 15 na kuzungumzia masuala kadha wa kadha yanayohusu shughuli za maendeleo baina ya nchi hizo mbili.
Mara baada ya mazungumzo na Mgeni wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amejitokeza kuongea na waandishi wa habari ambapo amesema katika mazungumzo yao wamegusia namna Marekani inavyoendeleza uhusiano kwa Tanzania katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Afya, Kilimo na masuala mazima ya Hifadhi za Taifa za Mikumi, Udzungwa na Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro amesema, Balozi Donald Wright amemhakikishia kuwaleta wawekezaji kutoka nchini Marekani kuja Mkoani humo kwa ajili ya kuonesha maonesho yanayolenga masuala mbalimbali ya kilimo.
Wakiwa kwenye mazungumzo kuhusu uhusiano baina ya nchi hizo mbili wawili hao wamezungumzia kuendeleza mahusiano hayo hususan kwa mwaka huu ambapo nchi hizo mbili zinaadhimisha miaka 60 tangu mahusiano hayo yalipoanzishwa mwaka 1961 kupitia kwa Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Rais wa 35 wa Marekani John Kennedy.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.