Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameaahidi kuanza ujenzi wa Barabara ya kutoka Bigwa hadi Kisaki Mkoani Morogoro kwa kiwango cha lami kwa kuwa ombi la kujenga barabara hiyo limetolewa na viongozi wengi na kwa muda mrefu.
Rais Magufuli ametoa aahidi hiyo leo Februari 12, 2021 mara baada ya kuzindua Kiwanda cha kusafisha na kufungasha mazao ya Mikunde cha Mahashree Tanzania Limited kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.
Ikiwa siku ya pili ya ziara yake Mkoani humo, Rais Magufuli kabla ya kufungua kiwanda hicho alifungua viwanda viwili kikiwemo kiwanda cha ngozi na kiwanda cha kukoboa mpunga na hatimae kuzindua kiwanda hicho cha Mahashree Tanzania Limite kilichojengwa kwa ajili ya kuchakata mazao ya jamii ya mikunde.
Amesema, ameamua kulibeba yeye mwenyewe ombi la kujenga barabara hiyo kwa sababu ombi hilo ni la muda mrefu na kwamba barabara hiyo inapitia maeneo muhimu na yenye watu wengi na utajiri Mkubwa, huku akiwataka watendaji wake wa ngazi ya Wizara kuanza kujipanga katika ujenzi wa barabara hiyo kwa awamu wakianza na ujenzi wa umbali wa kilometa 40.
Mhe. Rais amefikia hatua hiyo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mhe. Innocent Kalogeresi jana Februari 11 mwaka huu wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Morogoro kwa nyakati tofauti walimuomba Mhe Rais barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, Mhe. Rais amekubali ombi hilo ya kuahidi ujenzi huo kuanza baada ya Mbunge wa Jimbo la Morogoro kusini Mashariki Mhe. Hamisi Tale tale maarufu kama Babu Tale naye kuwasilisha ombi la ujenzi wa barabara hiyo na barabara ya Ngerengere kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuwa wananchi wa jimbo hilo wamekuwa na changamoto ya barabara hiyo kwa muda mrefu..
Awali akiwa katika kiwanda cha MW RICE MILLERS LTD, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kufufua kiwanda cha mafuta cha Moproco kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kisha kutafuta wawekezaji ambao watakiendeleza kiwanda hicho ambacho kimetelekezwa kwa zaidi ya miaka 20.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewataka watanzania wote kwa ujumla kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Watendaji wa Mitaa na Watendaji wa Vijiji katika zoezi la kuorodhesha majengo yanayotakiwa kulipiwa kodi kwa Serikali, zoezi ambalo litaanza nchi nzima kuanzia tarehe 15 hadi 28 mwaka huu.
Amesema, lengo la kulipa kodi hiyo kwa serikali ni kupata fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo ya nchi na wananchi mmoja mmoja kwa jumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amemuahidi Mhe. Rais kuendelea kuhamasisha wawekezaji ndani ya Mkoa na kuendeleza sera ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro amesema Mkoa huo hadi sasa una jumla ya viwanda 3,652, kati yake viwanda vikubwa ni 25, vya kati ni 16, vidogo 326 na vidogo sana ni viwanda 3285.
Akitoa salamu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Olesante Gabriel, amesema Wizara yake kwa sasa wamekomesha suala la wizi wa mifugo hapa nchini hususan wa ngo’mbe na kwamba wapo katika mkakati wa kupata njia mbadala ya kuwawekea ngo’ombe hao kifaa maalum katika miili yao ambacho kitasaidia kubaini ngo’mbe hao walipo endapo watakuwa wameibiwa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.