Barabara ya Morogoro - Dodoma kujengwa njia nne, nayo Mikumi – Ifakara yawekewa usimamizi wa karibu
Serikali imesema iko katika hatua za awali za kujenga barabara ya kutoka Morogoro kwenda Jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 267 kuwa barabara ya njia nne ili kurahisisaha usafiri na usafirishaji katika njia hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 2 mwaka huu na Msemaji Mkuu wa Serikali ndugu Gerson Msigwa wakati ikitoa taarifa ya wiki ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea wa kutoa taarifa hiyo kwa watanzania kila wiki.
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson msigwa akizungumza na waandishi wa habari wa Morogoro (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya Serikali katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro.
Msigwa amesema kwa sasa Serikali anamtafuta Mkandarasi mshauri ili kuanza hatua za awali za Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo kwa ajili ya kuipanua ili kuwa na njia Nne yaani njia mbili kwa kila upande.
Akifafanua zaidi, Gerson Msigwa amesema malengo ya Serikali katika kupanua barabara hiyo, kwanza barabara hiyo ndiyo inayounganisha maeneo ya katikati ya nchi, lakini pia inaunganisha mikoa ya kanda ya ziwa na ukanda wa magharibi mwa nchi yetu, aidha amesema ndiyo kiunganishi kikuuu cha nchi ya Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Kongo na kwamba ni muhim barabara hiyo ikaongezewa uwezo kwa kuwa inatumika kusafirisha mizigo inayokwenda katika nchi hizo jirani.
Katika hatua nyingine, Msemaji huyo wa Serikali amezungumzia ujenzi wa barabara ya Mikumi - Kidatu – Ifakara yenye urefu wa Km 66.9 kutoka Kidatu – Ifakara, pamoja na ujenzi wa Daraja la Ruaha Mkuu kwa kiwango cha lami.
Baadhi ya viongozi wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa morogoro (Morogoro Press Club - MORO PC) wakiwa katika picha ya pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali. kulia kwa Msemaji ni Mwenyekiti wa MORO - PC Nickson Mkilanya na kushoto kwake ni Katibu wa chama hicho Lilian Kasenene
Amesema, barabara ya Kidatu – Ifakara ni sehemu ya barabara kuu ya Mikumi - Kidatu - Ifakara - Mahenge/Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha yenye jumla ya urefu wa kilometa 547 amabayo inaunganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma na kudai kuwa barabara hiyo itakuwa na msaada mkubwa kwa watanzania wote lakini zaidi sana kwa wakulima wa ukanda huo hususan wa Bonde la Mto Kilombero na Mkoa wa Morogoro kwa jumla.
“Mradi huu wa kujenga sehemu ya barabara kati ya Kidatu na Ifakara kwa kiwango cha lami na Daraja la Ruaha Mkuu ni sehemu ya Mkakati wa Taifa kusaidia wakulima Wakubwa na Wadogo kupitia Program ya Uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania-SAGCOT, walioko katika Bonde la Mto Kilombero, ili kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao kipindi chote cha mwaka”. Amesema Gerson Msigwa.
Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Morogoro walioshiriki Mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali Oktoba 2 mwaka huu wakiwa katika picha ya Pomoja na Kiongozi huyo mara baada ya Mkutano huo.
Hata hivyo amesema barabara hiyo imekuwa inasua sua kwa muda mrefu kwani amesema hadi Julai 2021, Ujenzi wa Barabara hiyo ulikuwa umefikia asilimia 27 pekee ya Utekelezaji wake hali ambayo amesema Serikali haikufurahishwa hata kidogo na ucheleweshaji wa kukamilika kwa barabara hiyo.
Serikali baada ya kutambua tatizo, imechukua hatuaza haraka, ikiwa ni pamoja na Wizara kuagiza Usimamizi wa Mradi huo sasa ufanywe na Wakala ya Barabara kupitia Idara ya Usimamizi wa Miradi, TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU), baada ya muda wa mkataba wa Mhandisi Mshauri kukoma, Mwanzoni mwa Mwezi Agosti, 2021.
Afisa Habari, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Andrew Chimesela akiwa katika picha ya pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo hapa nchini Bw. Gerson Msigwa.
Serikali pia imemuonya Mkandarasi anayejenga barabara hiyo na kutakiwa kuongeza kasi ya ujenzi huo huku akiwekewa usimamizi wa karibu ili kukahikiasha kazi hiyo inakamilika mapema. Baada ya usimamizi huo kuchukuliwa na Wakala ya Barabara – TANROAD tayari mabadiliko yameanza kuonekana na kazi inakwenda kasi kwani hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu ujenzi huo umeshafikia asilimia 37.5.
Mwenyekiti wa Morogoro Press Club Nickson Mkilanya akiteta jambo na Msemaji Mkuu wa Serikali
Kazi ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara ulianza Oktoba 02, 2017, na muda wa Mkataba ulikuwa ni miezi 30, ambapo Mradi ulipaswa kukamilika tangu Aprili, 02, 2020 na Mkandarasi ameongezewa muda hadi tarehe 31 Oktoba, mwaka huu.
Ujenzi wa barabara hiyo unafadhiriwa na European Development Fund (EDF) kwa Ushirika na UKAID pamoja na USAID kwa gharama ya Euro 40,441,890.81 sawa na Shilingi za Kitanzania 120Bilioni.
kutoka kushoto ni Lilian Kasenene Katibu wa MORO PC na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Idda Mushi Mwandishi wa ITV na Redio One na Latifa Ganzel (Mhe. Diwani) na Mwandishi wa gazeti la Uhuru
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.