Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro wameiomba Serikali Mkoani humo kukomesha tabia ya baadhi ya watendaji wanaokukusanya fedha za mapato ya ndani bila kuziwasilisha sehemu husika na kusababisha kuibuka kwa hoja za Ukaguzi.
Ombi hilo limetolewa Juni 14, mwaka huu katika kikao maalum cha balaza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo kilicholenga kutoa majibu na mpango mkakati wa utekelezaji wa maoni yaliyotolewa na CAG kwa mwaka wa fedha 2019 – 2020.
Akiendesha kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Mhe. Rachael Nyangasi, amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa maelekezo ya kudhibiti tabia hiyo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU pamoja na Jeshi la polisi bila mafanikio yoyote.
‘’…Lakini Mkuu wa Mkoa wapo watu ambao tunawadai ambapo kikao cha mwaka jana kiliamuru TAKUKURU na Jeshi la Polisi kukamatwa kwa watu hao ambao wanadaiwa fedha lakini hadi sasa hawajakamatwa na hoja hii inaendelea…’’ amesema Nyangasi
Mhe. Nyangasi amesema Halmashauri hiyo inakwazika na hoja hiyo ambayo imeshindwa kutatuliwa kwa muda mrefu licha ya Halmashauri kuchukua hatua za kuwasimamisha kazi watendaji hao ambao walihusika katika ubadhirifu wa fedha katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Kwa Upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja, amesema watumishi wa Serikali ambao wamehusika katika ukusanyaji wa fedha hizo kisha kuzitumia kinyume na utaratibu wakatwe fedha kutoka katika mshahara yao baada ya hapo wafikishwa kwenye vyomba vya sharia.
‘’Tukate fedha zake kwenye mshahara kufidia pesa ambayo anadaiwa baada ya hapo tumpeleke kwenye kosa la jinai, haiwezekani afikishwe mahakamani kabla ya kuweka utaratibu wa kupata fedha zetu’’ amesema Mtunguja.
Akitoa maagizo kuhusu suala hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amewataka viongozi wa Halmashauri hiyo kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa wahusika wanaofuatilia mifumo ya fedha akiwemo mweka hazina, Afisa mapato na Mkurugenzi mwenyewe kuhakikisha watendaji hao wanapeleka benki fedha zote kila wanapokusanya.
Aidha, Martine Shigela, amewataka wanaosimamia madeni hayo kufuatilia fedha hizo ili wadaiwa waweze kulipa kwa wakati hivyo kuirahisishia Halmashauri ya Gairo kutokuwa na hoja kama hiyo kwa mwaka ujao.
Pamoja na maagizo hayo ameshauri kuwa kama wadaiwa hawatakuwa na uwezo wa kulipa madeni yao kutokana na mshahara wao kuwa mdogo watalazimika kuweka rehani mali zao kama nyumba, viali nyingine zenye thamani ya madeni yao ili kufidia pesa za Halmashauri.
Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali - CAG inaonyesha kufikia mwaka huu wa fedha 2019/2020 kuna zaidi ya shilingi Milion 21, fedha za Serikali ambazo zimeishia mikononi mwa watendaji.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.