Baraza la Vyama vya Siasa hapa nchini limewaonya na kukemea vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa kutumia vibaya majukwaa ya kampeni za siasa kwa kuhamasisha uchochezi na uvunjifu wa Katiba, Sheria za nchi na ukiukwaji wa maadili ya Kitanzania.
Agizo hilo limetolewa Machi 13, Mwaka huu na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bw. Juma Khatibu, wakati wa kikao cha siku mbili cha Baraza la Vyama vya Siasa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Nashera. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuvipa uwezo vyama vyote 19 vya siasa nchini.
Akifafanua zaidi, Bw. Khatibu amesisitiza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kuheshimu Katiba, Sheria za nchi, maadili ya vyama vya siasa, maadili ya uchaguzi na maadili mengine ya kitaifa ili kudumisha amani, utulivu na umoja wa Taifa.
"Baraza la Vyama vya Siasa linakemea vikali wanasiasa wanaotumia vibaya majukwaa ya siasa kuhamasisha uvunjifu wa Katiba, Sheria za nchi na maadili ya Kitanzania," amesema Bw. Juma Khatibu.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ameviasa vyama vya siasa kuwa na programu maalum za kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za siasa na kushika nafasi za uongozi.
Pia, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake katika kutetea haki za wanawake na kuwapa fursa za kiuchumi, kielimu na uongozi, kwani hatua hizo zinaendelea kuisaidia jamii.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa United Democratic Party (UDP), Bi. Saum Rashid, amewaasa wanasiasa kuandaa mazingira ya amani na utulivu kwa jamii kwa kuepuka mihemko na maneno yanayoweza kuleta mgawanyiko kwani uchaguzi ni chombo cha maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo kwa manufaa ya Taifa.
Naye, Katibu Mkuu wa Democratic Party (DP), Bw. Abdul Mluya, amewakumbusha wananchi kwenda kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kupata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu ili kupata viongozi wenye na maendeleo hapa nchini.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.