Viongozi wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya RS Morogoro pamoja na Viongozi wa TUGHE Taifa wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo Machi, 9 mwaka huu. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Baraza la TUGHE Taifa Dr. Mtungilwa, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala Bw. Herman Tesha na afisa bajeti kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Erick Ulomi.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro wamepitisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo takribani 11,873,795,000 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.
Bajeti hiyo imepitishwa Machi 9 mwaka huu na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro kwenye ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Afisa Bajeti Bw. Erick Ulomi akisoma mpango wa bajeti ya Baraza la wafanyakazi Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro kwenye ukumbi wa Mikutano uliopo Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akisoma mpango wa bajeti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro mbele ya wajumbe wa kikao hicho Afisa Bajeti kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Bw. Erick Ulomi amesema kati ya fedha hizo shilingi 8,079,813,000 zitaelekezwa kwenye matumizi ya kawaida ambayo yanajumuisha shilingi 3,776,918,809 kwa ajili ya mishahara na shilingi 4,243,316,000 ni matumizi mengineyo.
Aidha, Katika kikao hicho wajumbe wamependekeza suala la ajira kwa wafanyakazi wapya kwa kada mbalimbali lipewe kipaumbele ili kuziba mapengo ya watumishi yaliyotokana na kustaafu, kifo na kuhama kwani kasi ya kupungua watumishi kwa kila kada ni kubwa kuliko kasi ya kuajiri na hivyo kuathiri utendaji kazi katika ofisi mbalimbali.
wajumbe wa baraza la wafanyakazi Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye kikao cha kutoa mapendekezo ya bajeti ya 2023l2024.
Sambamba na hilo, wajumbe hao pia wameshauri Mkoa kujenga hoja na kuwasilisha hoja hizo ngazi ya Taifa ili kuongezewa Bajeti ya Mkoa kutokana na ukubwa wa Mkoa ukilinganisha na baadhi ya mikoa mingine pamoja na changamoto nyingine zinazojitokeza ndani ya Mkoa huo.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya UTAWALA aliwataka wajumbe wa kikao hicho kupitia kwa makini wasilisho la bajeti hiyo na kutoa maoni yao ili kuboresha bajeti hiyo kabla ya kuwasilishwa na kuidhinishwa na bunge lå Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Sekretarieti ya Mkoa huo iliidhinishiwa kutumia shilingi 11,873,795,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mmaendeleo, Kati ya fedha hizo shilingi 8,079,813,000 zilitengwa kwa ajili matumizi ya kawaida zilizojumuisha shilingi 3,836,497,000 kwa ajili ya mishahara na shilingi 4,243,316,000 matumizi mengineyo.
Mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo akichangia hoja wakati wa kikao hicho
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.