Zaidi ya Shiligi Bilioni 1.5 zimekopeshwa kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba Mkoani Morogoro ambapo watu binafsi, vyama vya ushirika na wajasiliamali wadogo wamekopa fedha hizo kwenye taasisi za kibenki kwa kutumia hati miliki za kimila walizopata kupitia mradi wa Matumizi bora ya Ardhi na kuwaendeleza kiuchumi.
Hayo yamebainika wakati wa kikao cha tathmini ya mradi wa matumizi bora ya Ardhi Land Tenure support Programu kilichofanyika Ifakara Wilayani Kilombero na kuhusisha Wilaya zilizopitiwa na mradi huo za Ulanga, Malinyi na Kilombero ambacho kiliongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo na wajumbe wengine wakiwa ni Watendaji wa Halmashauri hizo tatu pamoja na Maafisa wa Ardhi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba Mhandisi Stephano Kaliwa ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo wa urasimishaji Ardhi katika Halmashauri ya Mlimba kwani amesema umeleta manufaa kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na vikundi kupitia hati miliki hizo za kimila.
Akielezea zaidi kuhusu mafanikio hayo Mhandisi Kaliwa amesema hati za kimila zimeleta manufaa kwa wananchi wa Mlimba kwa kuzitumia kukopa fedha benki na kujiendeleza kibiashara huku akitolea mfano kuwa wafanyabiashara wadogo kwa ujumla ndani ya Halmashauri hiyo kupitia hati hizo wamefanikiwa kukopa shilingi milioni 150.
Akifafanua zaidi Mhandisi Kaliwa amesema wapo pia wakulima wa miwa wa Kijiji cha Msolwa Ujamaa ambao wamekopa shilingi milioni 300, na Serikali ya Kijiji hicho kukopa benki shilingi milioni 150 huku wafanyabiashara wengine wakubwa walifanikiwa kukopa shilingi milioni 900 kupitia hati hizo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa huo kufahamu kwa kina kazi zinazofanywa na Maafisa Ardhi wao kwa kila siku ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na hivyo kupunguza migogoro ya Ardhi Mkoani humo.
Aidha, Mhandisi Kalobelo ameagiza hati zote ambazo hazijatolewa kwa wananchi kwa sababu mbalimbali zitolewa kabla au ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu ili wananchi wazitumie hati hizo katika kuendeleza uchumi wao kwani hilo ndilo lengo la Serikali.
Nao wanufaika wa mradi huo ambao wamekopa fedha kupitia Taasisi za kibenki kwa kutumia hati zao za kimila akiwemo Logatha Ukota akiongea kwa niaba ya akinamama waliopata hati hizo ameiomba Serikali kuwapatia hati ya mtu mmoja mmoja ili mikopo watakayo ipata iwasaidie katika ujasiliamali mdogo.
Wajumbe wa kikao hicho cha siku moja walihitimisha kikao hicho kwa kutoka na maazimio mbali mbali ikiwa ni pamoja na kila Halmashauri kutakiwa Kubainisha watumishi ambao watapewa mafunzo ya namna ya kuendesha mfumo uliotumika katika kutekeleza mradi wa upimaji wa ardhi ili baada ya mafunzo waendelee kutekeleza kazi za upimaji wa ardhi katika maeneo yao ya kazi.
Maazimio mengine ni pamoja na Halmashauri zote za Mkoa huo kutakiwa kila mwaka kutenga bajeti ya kusimamia matumizi bora ya Ardhi lengo ni Mkoa kuondokana na migogoro ya ardhi, lakini pia kuhakikisha maeneo yote yaliyoainishwa kuwa na matumizi bora ya ardhi yanalindwa na kuendelezwa.
Hatua ya kufanya tathmini ya mradi huo imekuja baada ya uwepo wa dalili ya kupotea kwa manufaa yake ya Umilikishaji wa Ardhi, iliyofanyika kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa kutoka Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero ambazo ndizo zilipitiwa na mradi huo.
Tathmini iliyofanyika wakati wa kikao hicho, imeonesha kuwa kwa kiasi kikubwa malengo yaliyokusudiwa na mradi huo ya kupima mipaka ya Vijiji vya Wilaya hizo, kupanga matumizi bora ya Ardhi na kuratibu matumizi yenye maslahi kwenye vipande mbalimbali vya ardhi, yalifanikiwa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.