Tanzania na China zinaendeleza udugu wa siku nyingi kwa kupanga kufanyika kwa pamoja maonesho ya Utalii na Utamaduni ili kudumisha ushirikiano zaidi wa nchi hizo mbili kwa faida ya watu wa mataifa hayo.
Hayo yamebainishwa Disemba 5, 2023 na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Chen Mingjian alipofika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima na kufanya mazungumzo yakilenga kudumishi ushirikiano uliokuwepo kwa miaka mingi huku wakigusia ushirikiano zaidi katika sekta za kilimo na utalii.
Balozi Chen Mingjian amesema kuwa China na Tanzania zina uhusiano imara ulioanza tangu marais wa kwanza wa nchi hizo hivyo zimepanga kuendeleza umoja huo kwa uuandaa maonesho ya pamoja ya Utalii na Utamaduni ifikapo 2024. Lengo likiwa ni kukuza sekta hizo mbili za utalii na utamaduni na Kilimo.
Amesema, kwa upande wa Sekta ya Kilimo, China itashirikiana na Tanzania kuboresha reli ya TAZARA ambayo ndiyo kitovu kikuu cha njia kuu ya usafirishaji mazao kwa wakulima wa Mkoa wa Morogoro kupeleka Dar es salaam na nchi jirani kama vile Zambia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Balozi huyo kwa ujio wake ndani ya Mkoa wa Morogoro kwani anaamini kuwa Sekta ya Kilimo Mkoani humo inakwenda kukua.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema uwepo wa Reli ya TAZARA itasaidia wakulima wa Mkoa huo kusafirisha mazao yao kwenda sokoni hivyo ameishukuru Serikali ya China kwa kuwa na mpango mahususi wa kuiboresha reli hiyo.
Aidha, Mhe. Malima amemtaka Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na uzalishaji Mali Dkt. Rozalia Rwegasira kushirikiana na Mtaalam wa Mbegu kutoka nchini China ambaye ameanzisha shamba darasa la zao la Soya kuona namna ya kuhamasisha kilimo cha zao hilo kwa wakulima wengine.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaomba Wataalam hao wa Kilimo kutoka China, kushirikiana na uongozi wa Mkoa ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao mbalimbali likiwemo zao la Mkonge ambalo kwa sasa linazalishwa kwa wastani wa tani laki 6.
Ziara ya Balozi huyo wa China Mkoani Morogoro ilikuwa na lengo la kuangalia shughuli za Kilimo katika mashamba darasa yaliyopo vijiji vya Pea pea, Mtego wa Simba wilayani Morogoro na mashamba yaliyoko Mgeta Wilayani Mvomero.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.