Daraja la Dumila kutohamishwa, mbioni kuimarishwa.
Daraja la Dumila lililopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imebainika halitahamishwa kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali na badala yake litaimarishwa kuwa imara zaidi.
Hayo yamebainishwa na Waziri mwenye dhamana Mhe. Innocent Bashungwa wakati wa ziara yake aliyoianza Mkoani humo na kukagua daraja laDumila ambalo mara kadhaa limekuwa tishio kwa wasafiri wa barabara ya Dar es Salaam - Dodoma na mikoa ya kaskazini kwa sababu ya daraja hilo ujaa mchanga.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mhe. waziri, ili kutatua changamoto hiyo Serikali kupitia wataalam wa Wizara ya Ujenzi walifikia uamuzi wa kuchepusha barabara hiyo kupita eneo la juu la mto huo km 10 kutoka daraja lililopo sasa na kujenga daraja jingine.
Hata hivyo, Waziri ameagiza na watendaji wake kutochepusha barabara hiyo na daraja hilo kubaki mahali lilipo badala yake waliimarishe zaidi kwa kuwa tayari kuna uwekezaji mkubwa wa watu na Serikali katika mji wa Dumila.
Katika hatua nyingine Waziri huyo ameeleza pia namna Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutaka kupanua barabara ya mjini morogoro kutoka Kingolwila hadi kihonda ili kuondoa changamoto ya msongamano wa magari uliopo sasa.
Kwa sababu hiyo amemwagiza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROAD) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba kuanza kufanya tahmnini ya fedha zinazohitajika katika upanuzi wa barabara hiyo ili kuanza kutekeleza wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima ameendelea kuwaomba watu wa Dumila kuwa wavumilivu kutokana na kadhia ya maji yanayotokana na mto kuacha njia yake na kumwaga maji kwenye makazi ya watu na kwamba Serikalia ya awamu ya sita iko mbioni kushughulikia changamoto yao.
Hivyo ameendelea kumwomba Waziri wa Ujenzi wakishirikiana na Wizara ya Kilimo kuona uwezekano wa kujengwa mabwawa juu ya mto huo ili kupunguza kasi ya maji hayo na kutumika kwenye kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.