Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Mussa Kilakala ameyataka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali Mkoani Morogoro kufanya kazi kwa uwazi hususan katika kutoa taarifa za utendaji wao ili kuaminiwa na Serikali na jamii kwa ujumla hivyo kuleta mabadiliko chanya ndani ya jamii.
Ushauri huo umetolewa Agosti 28, 2024 na Mkuu huyo wa Wilaya akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akifungua jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoani humo lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Kiongozi huyo amesema kutokuwa na taarifa sahihi kunaathiri ufanisi wa usimamizi wa miradi na kusababisha hasara na upotevu wa rasilimali, hivyo ni jukumu la kila Shirika kutoa raarifa sahihi, kwa uaminifu na kwa wakati kwa maslai mapana ya Taifa.
"...Nasisitiza kuwa ni wajibu wa mashirika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa taarifa ili kuleta uaminifu na kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu...." amesema Mhe. Kilakala.
Mhe. Kilakala amesisitiza kuwa Mkoa wa Morgoro una julma ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali 499 ambapo 438 kati yake yanafanya kazi na mashirika 61 sawa na 12% yamesimamishwa kufanya kazi zao kwa kutokukidhi vigezo.
Amesema, mashirika 393 sawa na asilimia 90 ya mashirika yote yaliyohai (438) yanafanya kazi ngazi ya Taifa.
Akifafanua zaidi Mhe. Kilakala amesema, idadi kubwa ya mashirika yanayofanya kazi ngazi ya Taifa yanachangamoto katika utoaji wa taarifa na ufuatiliaji wa shughuli zao huku akinainisha kuwa baadhi ya mashirika hayo huhamisha Ofisi zao kwenda maeneo mengine bila kutoa taarifa, hali inayopelekea ugumu katika ufuatiliaji wa kazi zao.
Hivyo, ameyataka mashirika hayo kutumia jukwaa hilo kuweka mikakati bora zaidi na madhubuti ili kuondokana na sifa hizo zinazokiuka masharti ya usajiri wao.
Kwa upande wake Bw. Otanamus Nicholaus Mwenyekiti wa NACONGO Mkoa wa Morogoro amesema lengo la majukwa hayo ni kupeana taarifa, kujua changamoyo zinazoyakabili mashirika na kutoa elimu ya mambo yanayohusu NGOs.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo ametoa wito kwa mashirika hayo kufanya kazi zao kwa mujibu usajiri waliopewa, sheria za Nchi na kuwa wazalendo pamoja na kuisaidia jamii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira Bi. Sophia Kalinga amesema mashirika hayo yapo kwa lengo la kuisaidia Serikali katika utoaji wa huduma za kijamii na kuwaletea wananchi maendeleo yao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.