Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema kuwa Serikali ya Mkoa imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ndani ya miaka miwili, uzalishaji wa maziwa utachangia Shilingi bilioni 18 kwa mwaka katika uchumi wa Mkoa huo, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Mei 23, Mwaka huu, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu maadhimisho ya wiki ya maziwa kitaifa itakayoanza kufanyika kuanzia Mei 27 hadi Juni 1, Mwaka huu.
Amesema kuwa licha ya Mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe, bado hakuna uzalishaji wa maziwa wenye tija. Hata hivyo, tayari Serikali ya Mkoa imeweka mikakati ya kuhakikisha maafisa ugani wanatoa elimu kwa wafugaji ili kufanikisha uzalishaji wa lita 50,000 za maziwa kwa siku.
Kwa sababu hiyo, Mhe. Malima amezitaka taasisi za MORUWASA na RUWASA kupunguza gharama za uchimbaji wa visima ili wafugaji waweze kupata maji kwa urahisi, hatua itakayosaidia mifugo kutosafiri umbali mrefu kutafuta maji.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameishauri Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kuendelea kutoa elimu wakati wa wiki ya maziwa kuhusu njia bora za uzalishaji na uhifadhi wa maziwa, ili kuhakikisha maziwa yanayozalishwa yanakuwa yenye ubora na salama kwa matumizi ya binadamu.
Kwa upande wake, Afisa Teknolojia ya Chakula kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Rajilan Hilali, amesema Bodi hiyo imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa maziwa hapa nchini.
Ameongeza kuwa kwa mwaka 2024/2025, uzalishaji wa maziwa umefikia lita bilioni 4.01 kutoka kwa ng’ombe milioni 39 waliopo nchini, ingawa bado kuna changamoto ya uzalishaji kutokana na aina ya mifugo inayofugwa, hasa mifugo ya kienyeji.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.