Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima ameutaka uongozi wa Bonde la Wami Ruvu kuhakikisha wanaendelea na taratibu za kubaini vyanzo vya maji ndani ya manispaa ya Morogoro, kuchimba visima na kupata maji ili kuondoa changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Manispaa hiyo kwa muda mrefu.
Wito huo umetolewa Mei 24, 2025 na Mhe. Malima wakati alipotelembelea maeneo yaliyobainika kuwa ni vyanzo vya maji ambayo ni Maeneo ya Mafisa (Kaenzi) na Kata ya Tungi yaliyopo Halmshauri hiyo.
Mhe. Malima amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluh Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa mitambo kwa aajili ya kuchimba visima katika kila mkoa, hivyo kupitia kamati ya maji ihakikishe inaendelea na utafiti wa maeneo mengine huku maeneo yaliyobainika kuwa na vyanzo vya maji yaanze kuchimbwa na kusambaza maji kwa wananchi.
"... nimewaelekeza Bonde la Wami Ruvu waendelee kutafuta maji maeneo yale, haya maeneo tunayobaini kama tutapata maji kwa ujumla kama lita milioni 3 kwa siku tutaweza kupunguza adha ya maji.." amesema Mhe. Adam Malima
Kwa upande wake Meneja wa Idara ya Rasilimaji za Maji Bonde la Wami Ruvu Bw. Mrtin Daud Kasambara amesema maeneo yaliyobainika kuwa na vyanzo vya maji ni eneo la Tungi ambapo kisima hicho kinazalisha maji lita zaidi ya 23,000 kwa saa na eneo la mafisa ambapo kisima kitazalisha maji lita 30,000 kwa saa hivyo kusaidiq kupunguza adha ya maji kwa wananchi wa manispaa ya morogoro.
Naye mwananchi wa Kata ya Tungi Bw. Bululu Wai ameushukuru uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na Idara za maji kuhakikisha wanaondoa changamoyo ya maji katika eneo la Tungi amabapo eneo hilo wananchi wanakumbana na uhaba wa maji.
Imebainika kuwa wajumbe wa Kamati ya maji Mkoani humo ni pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) Bonde la Wami Ruvu, Maafisa ardhi wa Mkoa na Halmashauri pamoja na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.