Mkuu Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala leo Agosti 23 amerejesha hali ya taharuki kwa wafanyabiashara wa soko Kuu la Manispaa ya Morogoro la Chifu Kingalu baada ya viongozi wa soko hilo kulifunga kwa muda.
Madai ya wafanyabiashara wa soko hilo hadi kulifunga soko hilo ni kuwataka wafanyabiashara ndogo wa bidhaa za sokoni kutofanya biashara zao nje ya soko hilo badala yake warudi ndani ya soko ili wateja nao waweze kuingia ndani ili kununua bidhaa zao.
Mkuu Wilaya huyo akiongea na wafanyabiashara wa soko hilo sokoni hapo amewataka wafanyabiashara wote wanaofanya biashara zao nje ya soko hilo hususan wenye bidhaa zinazotakiwa kuuzwa ndani ya soko kuondoka barabarani mara moja na kuingia ndani ya soko hilo.
"..Mimi nikiwa na akili timamu siwezi kuruhusu watu kufanya biashara barabarani hilo halipo na halitatokea.." amesisitiza mussa Kilakala.
Aidha, amewataka mgambo wanaofanya kazi ya uangalizi wa taratibu zilizowekwa na Manispaa katika maeneo hayo wafanye kazi hiyo bila kuwapiga wala kuwanyanyasa wafanyabiashara hao wadogo kama Serikali ya awamu ya sita inavyosisitiza.
Amesema, kamwe Serikali haiwezi kuwanyanyasa wafanyabiashara ndogo kwa kuwa wamepunguza ukubwa wa tatizo la vijana kukosa ajira kwa wao kujiajiri.
Lakini pia amesema ajira hiyo inaondosha vibaka mitaani, wizi na vijana kujiunga na makundi yasiyofaa, hivyo ataendelea kukaa na viongozi wa kundi hilo la wafanyabiashara na wamachinga na kuhakikisha wanatekeleza yale wanayoyaomba.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Soko la Chifu Kingalu Bw. Halid Mkunyegere ametoa ombi kwa Mkuu huyo wa Wilaya la kupeleka stendi ya mabasi madogo maarufu kama daladala katika eneo la soko hilo kwa lengo la kuongeza ufanyaji wa biashara katika soko hilo ambapo Mkuu huyo wa Wilaya amelipokea ombi hilo na atalifanyia kazi.
Soko la Chifu Kingalu baada ya Maelekezo ya Mkuu wa Wilaya huyo tayari limeshafunguliwa na wafanyabiashara wa soko hilo wanaendelea na biashara zao kama kawaida.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.