Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Mussa Kilakala ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kushiriki Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal AID Campaign, yenye lengo la kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
ambayo itachangia kuimarisha Amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini.
Wito huo umetolewa leo Disemba 12 na Mkuu huyo wa Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake na kuweka bayana kuwa uzinduzi wa kampeni hiyo itazinduliwa rasmi kesho Disemba 13, 2024 katika viwanja vya stendi ya zamani ya daladala iliyopo katika Manispaa ya Morogoro kuanzia kuanzia saa 2:00 asubuhi, huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro.
Mhe. Kilakala amesema, kampeni hiyo inatekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji wa haki, mifumo ya utoaji haki, kuweka mazingira wezeshi yakulinda na kukuza haki ya upatikanaji haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini.
"..naomba kutoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro kushiriki uzinduzi huo ili kupata Elimu ya msaada wa kisheria tuweze kuzitatua kero na migogoro iliyopo bila ya malipo yoyote.." Amesisitiza Mhe. Mussa Kilakala.
Aidha, amesema mara baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo kukamilika, utekelezaji utaendelea katika Halmashauri zote 9 za Mkoa wa Morogoro na kila Halmashauri itafikiwa na huduma hiyo ndani ya Kata 10 na Vijiji 30 hivyo amewasisitiza wananchi kushiriki kwa wingi katika kampeni hizo katika kata zao ni vijiji au mitaa yao, lengo likiwa ni kukamilisha ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuwapatia haki ya msingi wananchi walio wanyonge.
Kampeni hiyo katika Mkoa wa Morogoro ambayo imejikita katika kuto elimu ya masuala ya kisheri itafanyika ndani ya siku 9 kuanzia Disemba 13, 2024 siku ya uzinduzi na inatarajia kutamatika Disemba 22, 2024.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.