DC Msando azitaka Halmashauri kufungua barabara
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kwenda kujikita kutafuata fedha kwa ajili ya kufungua barabara za mitaa/vitongoji kwa lengo la kutekeleza zoezi la anwani za Makazi linalotarajiwa kukamilika kabla au ifikapo Machi 30 mwaka huu ikiwa ni makubaliano ya ndani ya Mkoa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando akiongea na wajumbe walioshiriki kikao cha Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri MKuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alichokifanya kwa njia ya mtandao leo Februari 18, 2022
Albert Msando ametoa rai hiyo Februari 18 mwaka huu mara baada ya Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuahirisha kikao kazi cha viongozi wa Mikoa na Wilaya alichokuwa akikifanya kwa njia ya Mtandao ambapo kwa Mkoa wa Morogoro viongozi hao wamekutana katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Baadhi ya Wajumbe walioshiriki kikao hicho
Akiwa katika kikao hicho kilichohusu maendeleo ya maandalizi ya SENSA YA WATU NA MAKAZI ya mwaka 2022, Mkuu wa Wilaya Msando kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela amesema, ili anwani ya eneo moja iweze kukamilika lazima kuwe na barabara na barabara ili ifunguliwe kunahitajika fedha jambo ambalo amesema ndio jukumu lao la kwanza la kwenda kulifanya.
“lakini ili tuweze kwenda mbele lazima nguzo ya barabara iwepo, nguzo ya barabra ili iwepo lazima TARURA na Halmashauri zitambue barabara kwa sababu barabara lazima iwe formed, sasa maeneo ya vijijini ambayo ndio sehemu kubwa ya Mkoa wetu lazima tukaangalie hiyo changamoto kwamba…maana ili anwani ikamilike lazima kuwa na barabara” amesema DC Msando.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja kabla ya kuwaaga wajumbe walioshiriki kikao hicho, aliwataka Viongozi wote wanahusika na zoezi la Sensa ya watu na makazi ngazi ya Mkoa na Wilaya uhamasisha wananchi kwanza wajue maana ya sensa na faida zake na muda wa kufanyika zoezi lenyewe.
Aidha, katika kuhakikisha wanafanikiwa zaidi katika zoezi hilo, amewataka waratibu wa Sensa ya watu na zoezi la anwani za Makazi kutumia vyombo vya habari hususan vya Kijamii(Local Redios), nyumba za ibada ikiwemo misikiti na makanisa pamoja wazee wenye ushawishi ili kufikisha ujumbe huo.
Kuhusu zoezi la Anwani za Makazi, Katibu Tawala huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa ngazi ya Wilaya kuwasiliana na viongozi wa ngazi ya Mkoa pale inapotokea mgogoro ya Ardhi ambao kwao wanaona utaathiri zoezi hilo basi haraka wawasiliane na Kamishana wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Mashariki ili kuhakikisha wanaumaliza mgogoro huo kabla ya zoezi lenyewe kukwama.
sambamba na hayo, amewakumbusha Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kuwajibika kutumia fedha za mapato yao ya ndani kila wanapoona zoezi la Anwani za Makazi linakwama kwa sababu ya fedha na kwamba hilo ni agizo la Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sensa ya watu na Makazi ni zoezi muhim linalokusanya taarifa za kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya nchi usiku wa kuamkia siku ya Sensa, lengo ni kupata taarifa sahihi za kidemografia, Kijamii, Kiuchumina hali ya mazingira kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazowezesha Serikali na watu wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali.
Sensa kwa maendeleo, Jiandae kuhesabiwa
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.