Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli amewapongeza wananchi wa kata za Pemba, Diongoya na Kweuma Wilayani humo kwa kutoa mashamba yao 164 yenye ukubwa wa ekari 367.08 kwa ajili ya mradi wa urejeshaji hewa Ukaa unaoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la PAMS Foundation.
Mhe. Judith Nguli akipanda mti eneo la kitalu cha miti katika kata ya Pemba ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa PMS unaolenga kupunguza hewa ukaa.
Hawa ni baadhi ya wafanyakazi wakitayarisha vitalu vya miche kwa ajili ya kupandwa.
Mhe. Juditha amesema hayo Septemba 30,2023 wakati wa kukabidhi hatimiliki za kimila kwa wananchi 108 walioingia mkataba na shirika hilo la PAMS na mashamba hayo kutakiwa kupimwa na kuwamilikisha ili yaweze kutambulika kisheria.
Amesema, Ekari hizo 367.08 zitatumika kupanda miti itakayosaidia kurejesha uoto wa asili hivyo kupunguza wingi wa hewa ukaa hivyo amewapongeza na kubainisha kuwa kuyaingiza mashamba yao kwenye mradi huo ni kufanya biashara kama biashara nyingine itakayowaingizia kipato hapo baadae na kubadili Maisha yao kiuchumi.
Pamoja na shukrani hizo, amewataka wananchi hao kushika masharti ya mkataba walioingia na PAMS na kutotoa mashamba yao yote kwenye mradi huo ili maeneo yaliyobaki yatumike kwa matumizi mengine ya kiuchumi ikiwemo kilimo na kufuga.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji Mkoani Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira akipanda mti kwenye kitalu cha miti inayoandaliwa kwenda kupandwa eneo lenye ukumbwa wa ekari 367 kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mvomero Bw. Said Said akipanda mti eneo la kitalu cha miti kata ya pemba huku Mkuu wa Wilaya ya Mvomero na Afisa Mali Asili Mkoa wa Morogoro Bw. Joseph Chuwa (kushoto) wakishuhudia.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Christopher Maarifa akipanda mti eneo la kitalu cha miti Kata ya Pemba.
Afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Bw. Joseph Chuwa akiwa katika eneo la kitalu cha miti inayoandaliwa kwenda kupandwa kwa lengo kupunguza hewa ukaa.
Baadhi ya vitalu vya miche inayoandaliwa kwa ajili ya kupandwa
Katika hatua nyingine Mhe. Judith amelitaka shirika la PAMS kuwalipa kwa wakati fedha wanufaika walioingia nao mkataba ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza kwa kutotekeleza takwa hilo.
“cha msingi ni kuhakikisha malipo haya yanafanyika kwa wakati basi, hiyo lazima niwaagize PAMS, kwa wakati, ili tusiende kinyume na mkataba na ili msiwavuruge wananchi hawa” alisistiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Mratibu wa Mradi wa PAMS ndugu Richard Paul alitaja faida za mradi huo kuwa ni Pamoja na wananchi kupatiwa hatimiliki za kimila ili kumilikisha maeneo yao, kutoa ajira zisizo za kudumu kwa vijana 150 na kutoa elimu kwa jamii juu ya utunzaji sahihi wa mazigira.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli akimkabidhi hatimiliki ya kimila Diwani wa Kata ya Pemba Mhe. Coster Reuben.
Hapa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero akimkabidhi hatimiliki ya kimila Bi. Mariam Ally Mkazi wa Kijiji cha Pemba .
Faida nyingine ni kurejesha uoto wa asili kwa mashamba ya wanufaika kwa kupanda miti ambapo mwaka 2022/2023 zaidi ya miti 200,000 ilipandwa na kupitia mradi huo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imekusanya fedha zaidi ya shilingi 8,000,000/= kama ada ya usajiri wa hati 164 zilizotolewa kwa wanufaika wa mradi.
Kwa upande wao wanufaika wa Mradi wa PAMS wakiwakilishwa na Mwenyekiti wao ndugu Omary Hamza Kivumbi wamekiri kuupokea mradi huo kwa moyo na kwa hiari yao huku Bi. Mariam Ally akiwataka wanawake wengine kuhamasika kuingia kwenye mradi huo kupata hatimiliki ili wasinyanyasike kwenye ndoa zao.
Shirika la PAMS Foundation lilisajiriwa mwaka 2009 na lilianza shughuli zake za uhifadhi katika Mkoa wa Ruvuma na baadae Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Pwani, Manyara, Mbeya, Lindi, Dodoma, Tanga na Sasa Mkoa wa Morogoro.
Kwa Wilaya ya Mvomero Mradi huu upo katika vijiji vitano vya kata tatu za Pemba, Kweuma na Diongoya ambapo mradi umeanzia Kijiji cha Pemba ikiwa ni eneo ambalo linapatikana katika hifadhi ya Msitu wa Mkingu uliopo katika safu za Milima ya Tao la Mashariki yaani (Eastern Arc Montains).
Lengo la mradi huu ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kurejesha uoto wa asili kwa lengo la kupunguza wingi wa hewa ukaa na kuongeza kipato kwa wanufaika wa mradi kupitia miradi mingine kama kilimo Bora na chenye tija na kuunganishwa na masoko.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.