Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Mhe. Judith Nguli ameipongeza Benki ya Exim kwa kuunga mkono juhudi za Serikali Mkoani humo kwa kutoa vitanda 15 vya akina mama wajawazito ikiwa na lengo la kupunguza changamoto ya ukosefu wa vitanda kwa akinamama hao wawapo katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mhe. Nguli ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima, ametoa Pongezi hizo Julai 18, 2024 wakati akipokea vitanda hivyo 15 kutoka benki ya Exim na kuvikabidhi kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Magoma tukio lililofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema, msaada huo uliotolewa kwa akina mama ni moja ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Mkoa wa Morogoro na wadau mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"..Niwashukuru sana kwa namna ambavyo mnaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya hasa kwa upande wa kina mama .." amesema Mhe. Judith.
Aidha, Mhe. Nguli ametoa wito kwa wadau wa taasisi na mashirika mengine Mkoani humo kushirikiana na Serikali pale wanapoguswa waweze kutoa huduma kwa jamii ili kuweza kuujenga Mkoa wa Morogoro na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Magoma amesema licha ya kuendelea kupokea vifaa tiba mbalimbali kutoka Serikalini kuna upungufu wa vitanda 85 vya akina mama vya kujifungulia hivyo kupitia msaada huo kutoka Exim Banki vinaenda kupunguza adha ya ukosefu wa vitanda kwa vituo vya afya ambavyo havina vifaa hivyo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Exim Bank Bw. Stanley Kafu amesema wanatambua jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya ndio maana nao wamefikia hatua ya kuunga mkono sekta hiyo kwa kutoa msaada huo huku akibainisha kuwa msaada huo sio mwisho wa kuiunga mkono Serikali bali wataendelea kutoa misaada mingine katika sekta mbalimbali pale unapohitajika.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.