Wananchi wa Vijiji vya Ngaite na Tindiga Wilayani Kilosa ambako kuna mgogoro baina ya Jamii ya Wakulima na Wafugaji kugombania ardhi Block Na. 422 iliyoko ndani ya Lanch ya NARCO Mkoani humo, wametakiwa kuendelea kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji ndani ya Block hiyo kwa utaratibu utakaoelekezwa na Kamati itakayoundwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa hadi hapo Serikali itakapotoa maelekezo mengine.
Agizo hilo limetolewa Disemba 22 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare alipofanya ziara ya siku moja katika kijiji cha Ngaite Wilayani Kilosa ili kutatua mgogoro huo ulitaka kuhatarisha amani na utulivu kwa wananchi wa Vijiji vya Ngaite na Tindiga kutokana na kila upande kudai kuwa eneo la Block Na. 422 kuruhusiwa kufanya shughuli za kiuchumi za Ufugaji na Kilimo.
Loata sanare amesema wakati wanasubiri kuoneshwa mipaka na Maafisa kutoka NARCO, amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuendelea na kilimo katika mashamba yao ya zamani na kufugia kwenye maeneo ya awali pasipo kuazisha maeneo mapya ya mashamba au Ufugaji.
Katika hatua nyingine, Loata Sanare amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi kupitia Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kusimamia Amani na Utulivu wa eneo lenye mgogoro wa ardhi baina ya vijiji viwili vya Tindiga na Ngaite ili wananchi waendelee na shughuli za uzalishaji bila kubughudhiwa lakini bila kukiuka maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa.
“simamieni hilo, amani itokee, ng’ombe kwa mujibu wa viongozi wanasema watakuwa na shida sehemu ya kula lakini tumesema wale hivo mpaka mwafaka utakapotokea" aliagiza Loata Sanare.
Sambamba na agizo hilo Mkuu huyo wa Mkoa, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale kuunda Kamati huru ya kusimamia na kuhakikisha wakulima hao wanapata maeneo ya kulima pamoja na kulipia maeneo hayo, huku akimuagiza kuwa makusanyo ya fedha zote zinazotokana maeneo hayo kusimamiwa na Ofisi yake.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa NARCO ambaye alihudhuria kikao hicho, kwa niaba ya Meneje Mkuu Ndg. Mnzava Immanuel amekili suala hilo kutokamilika kwa muda uliopangwa na kuahidi zoezi la kuweka mipaka ya eneo lenye mgogoro kuanza kufanyiwa kazi mara baada ya sikukuu za Krismas na Mwaka mpya.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake Amina Kibuna ameiomba serikali kuharakisha uwekaji wa mipaka katika maeneo hayo kwa sababu muda wa kuandaa mashamba umefika ili kila mmoja awe huru kufanya shughuli zake kwa utulivu.
MWISHO
;
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.